Nimetembelea Songea (Ruvuma), na nimezurura mno.

Mji huu una hadithi kiasi, na nyingi pia; nilitembelea Makumbusho ya Majimaji na yale ya Simba wa Vita Baraka Mfaume Nyirenda tunayemfahamu kama Rashidi Mfaume Kawawa. Hapa Majimaji pana rekodi lukuki za vita, baadhi nitawashirikisha sasa au baadae kidogo. Nimepata mwenyeji mpya anaitwa Josefina, yeye ni mashuhuri hapa Mtini Bar ‘Yapenda Mtini’, na ni dada wa makamo ambaye ananisaidia sana kuhusu taarifa na habari kubwa za mjii huu.

Hapo baadae nitaenda Namtumbo kisha Mbamba Bay nikatazame Ziwa Nyasa kutokea upande ule.

Fahamu kuwa zipo meli zinatoka bandari ya Itungi (Kyela) huko nyumbani kwetu Mbeya hadi Mbamba Bay katika Ziwa Nyasa, fahamu zaidi kuwa ziwa Nyasa ni ziwa muhimu sana, kwanza ni moja ya maziwa kumi muhimu zaidi duniani (Top Ten) ambayo kwa tunu za Taifa letu na baraka za muumba sisi tunayo matatu; ikiwemo Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa lenyewe. Kwa Kiswahili kizuri, Tanzania ndio sehemu pekee duniani utakutana na maziwa matatu muhimu zaidi duniani kati ya kumi bila kuvuka mipaka yake.

Mashallah! Tuachane na Ziwa Nyasa kwa sasa.

Kwa uchache, hapa Songea pana Wangoni (Songea), Wayao (Tunduru), Wandendeule (Namtumbo), Wanyasa (Mbamba Bay) Wamanda (Nyasa/Mbamba Bay) na Wamatengo (Mbinga).

Josefina ananiambia hawa Wayao ambao ni wenyeji wa Tunduru ni mahodari na mahiri, anasema ni wale mabinti vigoli ambao msanii Mbosso huwaimba sana katika tungo zake. Umahiri huu umetokana na mafunzo ya umri na rika ambayo wao huita ‘kuchezwa’, ni sawa na mafunzo ya Jando na Unyago.

Hawa Wayao huchezwa mara tatu; ya kwanza ni pale anapopata mabadiliko ya mwili (hedhi), ya pili ni wakati anapokaribia kuolewa na mwishoni huchezwa pale anapopata uja uzito wake wa kwanza. Hii imewafanya Wayao wawe mahiri katika malezi yote; ya mume na familia.

Lakini Josefina si Myao hivyo itanilazimu nitafute rafiki wa kiyao nami nitazame kama nitawezana naye. (Utani)

Shukrani sana kwa Dullah Msabaha na Abdul wa Utengule Coffee Lodge kwa muongozo, wao walikwisha kufika hapa Songea siku za awali na wakapata nafasi za kutembelea maeneo mengi ya kitalii ambayo ni mahususi kwa wasafiri na wageni.

Nipende pia kutoa shukrani za dhati kwa watumishi wa Makumbusho ya Majimaji (Makumbusho ya Taifa) ndugu Emily Alex na Eric Soko ambao wametumia muda wao mwingi na elimu yao kunisaidia kupata ufahamu uliochagiza uandishi wa makala haya.

Siku za nyuma mimi na jamaa zangu tuliwahi kufika hapa Songea na kukaa kwa takribani miezi 2, ilikua Oktoba 2013 tarehe 22 tuliposafiri kuja hapa katika safari ngumu ya mateso nikiletwa hospitali ya Peramiho kwa ajili ya matibabu baada ya kuvunjika mguu huko Mbeya katika ajali ya gari 21/10/2013.

Kwahiyo, mimi na wenzangu tumekua tukifika hapa mara kwa mara, hata kwa shughuli zingine ukiacha hiyo ya matibabu. Klabu yangu ya Mbeya City FC ambayo mimi ni Ofisa wake wa Habari ina historia nzuri sana hapa Songea; kuanzia mechi ngumu za ligi daraja la kwanza na michezo mingine ya ligi kuu dhidi ya Majimaji SC. Wakati wote huo sikuwahi kusafiri kwa ajili ya Utalii hapa Songea. Hivyo, tofauti na safari zingine, hii ya sasa ni safari muhimu na nimeifanya kuwa spesheli mno; ndio maana nimesafiri mwenyewe ndani ya Tdi Landrover Defender 110. Wale ambao mmepanda au kuendesha 110 mnaujua ubora wake katika safari za mbali na raha za njia katika Tdi motion!

Nani amefika Ruvuma?

Well, Songea ya sasa si kama ile ya awali; pana tamaduni zilizochanganyika, na watu ni wengi pia. Pana kumbi, hoteli, hospitali na huduma tele za kijamii. Heko kwa Serikali ya watu wa Tanzania.

Bombi Nyumbi ni msemo mashuhuri sana hapa, kuna anayefahamu maana yake?

Za Kuyumka (Bwabina)

Jakudai (Jakuzibha)

Emonile (Safee)

Hizo ni sehemu ya salamu, sawa tu na zile Shinza Nyinza zetu Wasafwa au Ughonile za Wapwa zangu Wanyakyusa.

Karibuni Songea Karibu Majimaji Karibu Matimila!

Hapo awali nilieleza kuwa nitawashirikisha kiasi kuhusu Majimaji na Songea kwa kifupi, sasa kuelekea lunch ninaomba niwape muhtsari kidogo wa Majimaji na mji huu kwa ujumla wake, na nitatumia picha kufafanua maelezo.

Nitaanza na Chief Msaidizi Nduna Songea Luwafu Mbano. Hii hapa chini picha yake.

Nduna Luwafu Mbano alikua Chief Msaidizi na Mwandamizi kati ya Machifu 12 wa Chifu Mputa Bin Gwazerepasi Gama. Huyu Mputa alikua Chifu Mashuhuri wa Mji huu ambao awali ulijulikana kama Ndonde. Wakati wa ukoloni kutawala ardhi yetu kwa mabavu, hapa Songea Wajerumani waliua wapiganaji wengi wa Majimaji, wakiwemo Machifu.

Muonekano wa Mji wa Ndonde (Songea)


Hawa pichani ni sehemu ya mashujaa wa vita vya majimaji muda mfupi kabla ya kunyongwa tarehe 27.02.1906.

Hili ni kaburi la jumla (Mass Grave) la mashujaa wetu walionyongwa siku moja ya tarehe 27.02.1906, kaburi lao lipo hapa kumbukumbu ya Majimaji.

Chief Msaidizi Nduna Songea Luwafu Mbano hakunyongwa siku hiyo ya 27.02.1906, watawala wa mabavu wa Kijerumani walitaka wamtumie kama kibaraka ili kuendeleza jitihada zao za kifashisti za kuwakandamiza kwa kuwatawala waswahili wenzetu.

Haya ni majina ya mashujaa 66 walionyongwa siku hiyo, isipokua Chief Msaidizi Nduna Songea Luwafu Mbano.

‘Ninyongeni siwezi kuishi katika dunia hii, wenzangu tayari wamenyongwa’. – Chief Msaidizi Nduna Songea Luwafu Mbano

Tarehe 02.03.1906 Chief Msaidizi Nduna Songea Luwafu Mbano alinyongwa baada ya kukataa kushirikiana na Wakoloni kuwakandamiza waswahili wenzetu, kwahiyo alinyongwa na kitanzi lakini kilikatika mara tatu wakati akinyongwa. Hivyo Wajerumani wakaamua kumuua kwa risasi.

Hili ni kaburi la Chief Msaidizi Nduna Songea Luwafu Mbano, tofauti na wenzake walionyongwa ile tarehe ya awali, yeye alipewa heshima na kuzikwa peke yake. Hivyo, alizikwa kwenye kaburi la pekee lililo jirani na mti wa asili uitwao ‘Chikunguti’. Na kutokana na ujasiri wake vitani, Wajerumani wakampa hadhi, mwaka huo huo wakabadili jina la sehemu ya Ndonde kuwa Songea, na sasa ni Halmashauri ya Manispaa ya Songea. Mji huu wa Songea ulijulikana kama Ndonde awali, jina la Songea limetokana na Chief Msaidizi Muandamizi Nduna Songea Luwafu Mbano.

Huyu Chief Msaidizi Nduna Songea Luwafu Mbano kama waswahili wengi wangekua wanaandika na kuchapisha, basi tusingepaswa kabisa kuzijua hadithi za Goliath na Daud, hizi zilitosha sana kuamsha Uafrika ndani yetu.

Kwahiyo, jina la Songea limetokana na mbabe huyu wa Vita Chief Msaidizi Nduna Songea Luwafu Mbano.

Nilipiga picha mbele ya mnara huu wa askari ambapo pia ipo minara ya sanamu iliyoundwa kwa jailli ya kumbukumbu za mababu zetu waliopigana katika vita via Majimaji. Minara huu ni alama ya ushujaa nami nimejipa jina jipya Nduna Shah Mjanja Mbano kama mashujaa wenzangu wa Majimaji.

Katika huu mnara huu mkubwa yapo maandishi ya kishupavu, muhimu na yenye kuvutia mno. Ukiacha misemo ya akina Solomon Mahlangu au Bob Marley, mashujaa wa Majimaji nao wametuachia misemo yenye tija na maana.

‘SISI MABABU ZENU MASHUJAA WA MAJIMAJI TUMETOA MAISHA YETU KUTETEA TAIFA LETU, TUMETIMIZA WAJIBU WETU ULIOBAKI NI WENU’

Hizi ni silaha za jadi za Majimaji na hii picha ni silaha halisi na mchoro huu wa pembeni unaonesha namna gani silaha zilivikwa mwilini tayari kwa vita

Kitanzi cha kunyongea

Mnara wa askari

Maingilio ya makumbusho ya Majimaji

Tofauti na site nyingi nilizotembelea, mfano maporomoko ya Kaporogwe au Isimila Stone Age; ukiacha Hifadhi za Taifa, haya makumbusho ya Majimaji ni sehemu nzuri iliyohifadhiwa kuliko zote nilizowahi fika.

Hapa ndani pia nimekutana na bookshop ya Makumbusho ya Taifa, na nimejinunulia nakala chache zikiwemo.

  1. Zamani: Hiki kinaonesha maisha ya zamani katika zama muhimu

2.Tanzania: Hiki kinaonesha kwa kina na kwa picha, tamaduni zetu zikiwemo tabia mila na desturi.

  1. Mtanzania wa Kale: Hiki kinafana na Tanzania
  2. Mpira wa Miguu Tanzania: Namna gani mpira ulisaidia harakati za ukombozi
  3. Simba wa Vita; R. M. Kawawa

Hiki cha Kawawa kimenifurahisha sana, ninajisikia Amani kuwa na kitabu cha Mswahili mwenzangu tena mashuhuri. Kabatini kwangu nina Azimio la Arusha la Mzee Nyerere, hii inaenda kuwa hazina ingine.

Hiki cha mpira kitakuza fikra zangu na uelewa wa Mpira katika zama za kale.

Humu ndani zipo picha za Mzee Nyerere, Karume, Kawawa na wadau wengine wengi hapo zamani wakitazama soka. Mpira ulikua ni sehemu muhimu sana ya kujumuisha siasa kabla ya Uhuru, kumbuka kuwa mikutano na maandamano hayakuruhusiwa wakati huo. Kwahiyo mpira ulikua ni jukwaa muhimu.

Katika hiki kitabu, uwanja wa Ilala, ambao sisi sasa hivi tunauita uwanja wa Karume umetajwa sana, ni jambo la kushangaza ya kuwa uwanja wa Karume si uwanja unaotajwa sana kwa sasa licha ya kuwa ofisi adhimu za Shirikisho la Mpira zipo ndani yake!

Hii ndiyo dawa yenyewe ya Majimaji iliyoaminika kuyeyusha risasi za mkoloni. Mchanganyiko huo ni hatari sana kwa afya ya adui na silaha za kimagharibi. Nitaiba kila dawa kidogo, kwenye party za Everyday Mbeya (@everydaymbeya) nitakua nakuja na masabweka wenzangu wa Kisafwa kuwachanja na dawa hii! (Utani)

Mtagundua kuwa hadithi za masimulizi ya kumbukumbu ya Majimaji nimezizungusha kwa Chief Msaidizi Nduna Songea Luwafu Mbano, Yes! Hilo liilikua lengo langu, lakini yapo makumbusho ya Kisasa yanajengwa na Makumbusho ya Taifa hapa Songea.

Nimepewa kibali kutembelea makumbusho haya, ni makumbusho mahususi kwa ajili ya Mzee wetu Kawawa, lakini bado yapo katika Ujenzi chini ya TBA.

Baadae, nitawaeleza zaidi kuhusu huyu Simba wa Afrika.

Lakini kwa uchache, siku 45 baada ya uhuru wa Tanganyika; Mwl Nyerere alimwachia nefas i Mzee Kawawa kuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika. Mwalimu aliachana na wadhifa huo ili apate muda wa kujenga chama chake cha Tanganyika African National Union (TANU).

Mwaka mmoja baadae Desemba 1962, Kawawa alikubali kuunda Jamuhuri ya Tanganyika na kuridhia Mwl. Nyerere kuwa Raisi wa Tanganyika.

Nani katika umri wetu atakubali? Sisi vijana wa 1982 tutaweza?

Kwahiyo, Kawawa ni mtu nadra sana, na kwao ni Namtumbo hapa Ruvuma. Pongezi kwa Makumbusho ya Taifa kwa kutunza vema kumbukumbu za Taifa letu.

Kwahiyo Songea ina mashujaa, wengi, wakiwemo Chief Msaidizi Nduna Songea Luwafu Mbano na Mzee Rashid Mfaume Kawawa aliyejulikana kama Simba wa Vita, jina alilopewa na Mwalimu. Fahamu kuwa yupo gwiji mwingine mwanamuziki hodari Remmy Ongala ana rekodi tele hapa, si Mzawa lakini ni mashuhuri jukwaani, kuanzia kwa Matimila mwenyewe aliyeanzisha naye Super Matimila Band. Taarifa zaidi kuhusu Ongala ‘Mambo kwa Soksi’ na Songea zitafuata hapo baadae.

Alamsiki!

Makala hii imeandikwa na Shah Mjanja.

Shah Mjanja ni mpiga picha wa muda mrefu, Muandishi na Mtayarishaji wa makala za televisheni na filamu, Mhifadhi, Mwanamuziki na Msafiri. Ni muanzilishi wa Everyday Mbeya na Studio Native.

Shah Mjanja ni Ofisa wa Habari za klabu ya Mbeya City FC.

Mawasiliano:

Simu: +255-682-326410
Barua Pepe: shah@everydaymbeya.com

 

Sindikiza makala haya kwa kusikiliza kibao chake Remmy Ongala – Narudi Nyumbani.