Tarehe 22 March 2018 nilichukua safari ndefu lakini fupi, kutoka Mbeya mjini ninapoishi kuelekea Masoko kutazama ziwa maarufu la Kisiba. Safari ile ya kilomita takribani 80 haikuchosha kwa muungurumo wa Landcruiser mahiri iliyoungurumishwa na Seleman tunayependa sana kumuita ‘Mnyama’ kutokana na ubobezi wake katika udereva.

Sikua mwenyewe katika gari, nilikua na Afisa Utalii wa Rungwe ndugu Numwagile Arthur na Judith Kibona ambaye ni ofisa wanyamapori wa mkoa wa Mbeya. Pamoja nasi alikuwepo Ridhiwani Gambalela ambaye ni Ofisa wa habari wa wakala wa huduma za misitu nyanda za juu kusini, yeye pamoja na Seleman ‘Mnyama’ wanahudumia Mount Rungwe Nature Reserve, lakini alikuwepo pia Daniel Mwakasungula  wa Studio Native; moja ya Studio za picha zinazotoa huduma kwa wakaazi wa Mbeya na kwingineko.

Mji wa Masoko unaonekana kuwa mji mkongwe kutokana na masimulizi lakini hasa kwa majengo yaliyopo ambayo yalitumika kama ofisi za serikali zote mbili za kikoloni (Ujerumani na Uingereza) kuanzia miaka ya 1886. Mji huu unapewa nakshi na asili ya tamaduni zake, maumbile ya ardhi, uoto wa asili na muonekano wa milima ukiwemo mlima Rungwe. Katika mji huu ndipo linapopatikana Ziwa Kisiba ambalo wengine huliita Ziwa Kisiba Masoko au Ziwa Masoko.

Ziwa Kisiba ni ziwa la volkano ambalo kisayansi limetokana na mlipuko wa volkano, lina upana wa mita 600 na kina chenye mita 70. Ziwa hili ni salama kwa kuogelea na michezo mingine ya ziwani kama Boat Cruising, Camping, Sport Fishing na mingine mingi.


Ziwa Kisiba kutokea Juu.


Familia ya kikoloni ikiogelea katika ziwa Kisiba.


Wasafiri wetu wakiogelea juu ya ziwa Kisiba.

Tulipofika Ziwa Kisiba tulilakiwa na Ofisa Mtendaji wa eneo hilo, fahamu kuwa ziwa hili linasimamiwa na Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe ambao wana jukumu la kutunza, kutoza tozo za wageni na kuendeleza ziwa hili. Tulifanya mahojiano na Ofisa Mtendaji na Mzee mmojawapo mkaazi wa ene hilo.


Judika kibona, Afisa wanyamapori; mbele ya jengo la kikoloni.


Numwagile na Judika mbele ya Jengo la kikoloni.

Haya majengo ya kale yalitumiwa na serikali za kikoloni kama Ofisi za utawala, mahakama na shughuli zingine za kiofisi, kwa sasa majengo haya yanaendelea kutumiwa na Halmashauri ya Rungwe kwa shughuli zile zile za kiutawala.

Baada ya matembezi haya nilishangazwa sana na uzuri wa ziwa hili, na kisha nikawa na kiu isiyokata ya kutaka kuwaleta rafiki zangu, nao waje waone uzuri wa nchi. Hivyo, nilishirikiana na Everyday Mbeya kuandaa safari ya kitalii kwa ajili ya mafunzo, burudani na matembezi.

Kwa nyakati mbili tofauti Everyday Mbeya ilileta wasafiri wa makundi kutoka maeneo mbalimbali hapa ziwani Kisiba, na mara kadhaa wageni binafsi. Matembezi katika safari hizi zote yalisaidia kuwafahamisha watu wengi uzuri wa ziwa Kisiba.

Katika safari zote hizo zilikuwepo changamoto kiasi, mfano ziwa halikuhudumiwa ipasavyo na halmashauri, na liliondolewa ubora na watumiaji wakaazi. Mara kadhaa unaweza kufika ziwani na kukuta maji yamejaa mapovu ya sabuni kutokana na shughuli za wakaazi zikiwemo kufua, kuosha vyombo na pikipiki na mengineyo. Ziwa Kisiba lilitengeneza muonekano mzuri katika picha lakini ulipofika huenda ukashangazwa na mandhari inayolizunguka.

Kisiba Campsite

Kwa sasa ziwa Kisiba linapendeza zaidi hasa baada ya kupata muwekezaji ambaye amejenga Campsite inayosaidia kupokea wageni wa kutwa na wanaolala. Huduma za wasafiri zimeboreshwa kwa upatikanaji wa miundombinu kama maliwato, kioski, viti na maturubai (tents) ya kulalia wakati wa usiku. Lakini pia ujenzi wa miundombinu hii ziwani inawavutia zaidi wasafiri wengi kutembelea ziwa Kisiba.


Lango la Kisiba Campsite


Muonekano wa Ziwa Kisiba kutokea Campsite


Sehemu ya moto wakati wa usiku


Kioski cha vinywaji na chakula


Viti vya kunywea vinywaji juu ya mti


Gati pembeni ya maji

Campsite hii imefanya ziwa Kisiba liwe bora hata zaidi na zaidi! Ukihitaji kufika unaweza wasiliana na msimamizi wa Campsite kwa nambari hii +255 756 929 868. Kisiba Campsite hutoza kiasi cha shillingi 3,000/- kwa wageni. Huduma za chakula huenda zikapatikana kwa kuweka taarifa ‘booking’ mapema. Kwa matembezi mazuri zaidi unaweza kujibebea baadhi ya vitu utavyohitaji, huenda chaguzi za vitu spesheli kama Hennessey au Pizza zisipatikane.


Ukifika Kisiba utakutana na hawa vijana wawili, ni wacheshi mno na watafanya safari yako kuwa nzuri zaidi kwa masimulizi, ukarimu na huduma. Usisahau kuwapatia ‘tip’ baada ya mapumziko yako.

Hadi naondoka Kisiba nilipotembelea tarehe 08 Februari 2021 nilishuhudia marekebisho ya barabara itokayo Tukuyu Mjini kuelekea Masoko lilipo ziwa Kisiba, lakini, licha ya kuwa barabara hii huhudumiwa mara kwa mara huenda ukahitaji gari imara zaidi unapohitaji kutembelea hasa wakati wa mvua. Maji ya mvua hufanya barabara iteleze sana na kuweka mashimo na matope mengi.

Kwa namna nyingi mji wa masoko umenipatia marafiki wengi lakini hasa wazee wangu wawili wanaojulikana kama Joshua na Brados, na kila mara napoenda ziwani huwa namkumbuka Mzee wangu Joshua ambaye siku za kale alikua maarufu kwa jina lake Dj. Jerry au King Dj. Jerry.


Kushoto: Brados, Shah Mjanja. Msimamizi Ziwa. Hance Njobelo na Dj. Jerry (Mzee Joshua)

Dj. Jerry na kaka yake Brados wamefanya maonesho na kutumbuiza katika bendi yao ya familia iliyojulikana kama Ochestra Bana Africa. Jerry alikua muimbaji, mpiga gitaa na mtozi katika bendi yao.

Orchestra Bana Africa ilikua bendi ya muziki iliyotumbuiza huko Arusha, Nairobi na Dar es Salaam kati ya mwaka 1970 hadi 1978, lakini pia walifanya maoensho katika miji mingine kama Babati na nyumbani kwetu Kondoa. Walikua maarufu, na waliimba pia kwa lugha za kigeni ikiwemo kiingereza.

Mzee Joshua ameisaidia sana Everyday Mbeya kufanya safari zake ziwani Kisiba, ameungana nasi wakati wote wa shughuli na amekua akiwapokea wageni wetu kwa furaha tele. Mzee Joshua (Dj. Jerry) amekua akitupa Masada wa hali na mali kuanzia maandalizi hata wakati wa shughuli zote, kuanzia mwanzo hadi mwisho.

Mzee Joshua anaishi na familia yake akiwemo kaka yake Brados kijijini masoko jirani kabisa na ziwa, ukitembelea ziwani usisite kumuulizia na kumfikishia salamu zangu za dhati.

Wasalaam,

Makala hii imeandikwa na Shah Mjanja.

Shah Mjanja ni mpiga picha wa muda mrefu, Muandishi na Mtayarishaji wa makala za televisheni na filamu, Mhifadhi, Mwanamuziki na Msafiri. Ni muanzilishi wa Everyday Mbeya na Studio Native.

Shah Mjanja ni Ofisa wa Habari za klabu ya Mbeya City FC.

Mawasiliano:

Simu: +255-682-326410
Barua Pepe: shah@everydaymbeya.com

 

Kama kawaida yetu, nakuachia wimbo huu ukuliwaze baada ya kusoma makala haya.