Mkoa wa Mbeya ni moja kati ya mikoa minne (4) iliyopo katika Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania. Mikoa mingine ni Rukwa, Iringa na Ruvuma. Mkoa wa Mbeya ulianzishwa mwaka 1961 na ulikuwa ukijulikana kwa jina la ‘Southern Highland Province’ kwa kujumuisha baadhi ya maeneo ya mikoa ya Iringa na Rukwa. Mkoa una eneo la km. za mraba 63,617 Kati ya hizo km. za mraba 61,783 ni za nchi kavu na km. za mraba 1,834 ni eneo la maji. Kulingana na Sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 1967 mkoa ulikuwa na watu 969,053, Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002 Mkoa wa Mbeya ulikuwa na jumla ya watu 2,063,328.

Kufikia mwaka 2010 mkoa ulikadiriwa kuwa na watu 2,662,156. Mkoa wa Mbeya upo kusini magharibi mwa eneo la Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania. Mkoa upo katika Latitudi kati ya 7º na 9º 31’ kusini ya Ikweta na Longitudo kati ya 32º na 35º mashariki ya Greenwich. Mkoa unapakana na nchi za Zambia na Malawi upande wa kusini, Mkoa wa Rukwa upande wa magharibi, Mikoa ya Tabora na Singida kwa upande wa kaskazini ambapo kwa upande wa mashariki unapakana na Mkoa wa Iringa. Mji wa Tunduma katika Wilaya ya Mbozi na Kasumulu katika Wilaya ya Kyela, hufanya milango ya kuingilia na kutokea nchi za Zambia na Malawi.

Katika enzi za ukoloni wa Waingereza, Mkoa wa Mbeya ulikuwa ukijulikana kwa jina la ‘Southern Highland Province’. Mkoa ulikuwa ukiunganisha baadhi ya maeneo ya mikoa mitatu ya sasa ambayo ni Iringa na Rukwa. Jina la Mbeya limetokana na neno la kisafwa.”Ibheya” ambalo maana yake ni chumvi, kutokana na wafanyabiashara kufika.na kubadilishana mazao yao kwa chumvi.

Mji wa Mbeya ulianzishwa na wakoloni Waingereza mnamo mwaka 1927. Wakati huo dhahabu ilianza kupatikana katika milima iliyopo karibu na Mbeya hadi Chunya hivyo Mbeya ulikuwa ni mji wa mapumziko kwa Wazungu kutokana na hali yake nzuri ya hewa, hali iliyosababisha mji wa Mbeya kupewa jina la utani kama “The Scotland of Africa” baada ya kutambua kama uoto, hali yake ya hewa na muonekano wa milima (hills) inayouzunguka mji wa Mbeya kufanana na Scotland mfano uoto unaopatikana katika mlima Loleza. Mkoa huu ni moja kati ya mikoa mikongwe
iliyokuwepo mpaka wa kati wa uhuru mwaka 1961. Katika kipindi hicho, makabila makuu katika Mkoa wa Mbeya yalikuwa ni Wasafwa, Wanyakyusa, Wandali, Wasangu, Wamalila, Wanyiha, wakimbu na Wanyamwanga. Ambapo jamii hizo ni maarufu kwa kujishughulisha na kilimo na ufugaji mdogomdogo.

Source: www.mbeya.go.tz