Hello Everyday Mbeya,

Yapo maeneo machache sana duniani ambayo unaweza kukutana na Satari Mola wetu Msitiri, mara kadhaa nimekua nikiyataja maeneo haya pale Access FM [100.9MHz] kupitia kipindi chetu cha Utalii kinachojulikana kama Everyday Mbeya. Sehemu mojawapo Katika maeneo hayo ni Kitulo, na nimekua nikiwaeleza mara kwa mara wasikilizaji wetu, ni kwanini Kitulo?

Fahamu kuwa Kitulo inapatikana kwa sehemu kubwa mkoa wa Njombe wilaya ya Makete na mkoa wa Mbeya.

Sasa, kwanini hatuendi Kitulo wakati wa dry season?
Au tuseme kwanini tunaenda Kitulo wakati huu wa mwisho wa mwaka?

Well, kabla sijasema kitu hebu mtazame kwanza msanii Freshley Mwamburi na kibao chake cha ‘Stella Wangu’, wimbo huu ni mahususi kwa wana Everyday wote wanaoisoma makala hii wakiwa njiani kwenda kutalii maeneo yoyote ndani ya Taifa letu, na wimbo huu uliimbwa kwa umahiri sana na Rafiki yetu Priscus Kimario wakati wa safari yetu moja, usiku wa manne katika fukwe za matema 🙂

Siku za nyuma nilifanya tafakari ya kufanya Utalii hifadhini Kitulo wakati ambao si ‘fevarabo’ kama ambavyo wengi wamekua wakisema, lengo langu ilikua kuona ni nini mgeni atafanya na kufurahia ndani ya hifadhi hii adhimu Africa katika kipindi cha kiangazi. Kwa bahati mbaya sikufanikisha safari hiyo, hivyo basi kwa kuwa masika yapo jirani, nakupa dodoso kadha wa kadha na kukuwezesha ujifunze kwanini hifadhi ya Kitulo ni lazima kwako wewe msafiri kutembelea.

Kwanza, inashangaza kuwa licha ya kuwa hii ni hifadhi muhimu kutokana na ikolojia yake, bado si hifadhi inayotembelewa sana na wazawa, mhhhh, ndiyo.

Pili, inavutia namna gani Kitulo inawashangaza watu wote waliofika hifadhini kwa kujua ama kutokujua.

Twende hifadhini sasa 🙂

1. Hali ya Hewa

Ulimsikia Waziri wetu wa Utalii aliyoyasema kuhusu Utalii wa hali ya hewa?

Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ni hifadhi iliyo juu zaidi nchini Tanzania katika muinuko wa mita 2500 hadi 3000 juu ya usawa wa bahari, hali hii inaifanya Kitulo kuwa na joto la chini zaidi kati ya nyuzi 7 hadi 8 katika miezi ya Disemba hadi Aprili, na licha ya kuwa hifadhi hii hupata joto kwa takribani nyuzi 14 hadi 18 wakati wa kiangazi, bado baridi yake ni kali sana na kushangaza wageni wengi hasa kutoka ndani ya Afrika.

Hali hii imefanya wasafiri waliofika Kitulo kuitambua kama Scotland ya Afrika kutokana na kiwango cha chini zaidi cha joto katika meizi ya Juni hadi Agosti. Hiki ndicho kipindi ambacho joto hushuka zaidi hadi nyuzi 0.5 na kushuhudiwa kwa theluji ndani ya hifadhi.

Fahamu kuwa Kitulo ni mojawapo ya hifadhi 22 za Taifa, je? Wewe umefika hifadhi ngapi nchini?

2. Maua

Sifa mojawapo tena yenye upekee kuhusu Kitulo ni MAUA yanayomea ndani yake, hii ndio imewafanya wajuzi wa mambo waiite ‘Bustani ya Mungu’. Hifadhi ya Taifa ya Kitulo imesheheni ustawi maridadi wa maua mazuri tena yasiyo kifani, duniani huwa tunaiita  ‘The Serengeti of Flowers’.

Mwaka fulani nilichukua kamera na kujaribu kupiga picha maua ambayo nilikutana nayo kwa wingi ndani ya hifadhi ya Kitulo. Hebu jionee mwenyewe uzuri wake.

Ukiwa Kitulo unakua katika moja ya maeneo mazuri ya maua ya asili duniani, ambayo kati ya hayo, kuna zaidi ya aina 40 za maua ya Chikanda, ambazo aina 31 zinapatikana Tanzania tu, aina 16 katika hifadhi ya Kitulo na milima ya Uporoto na aina 3 hupatikana ndani ya Kitulo pekee.

Uanda wa maua haya unaifanya Kitulo iwe the best destination in Afrika.

Ni maua gani yanaipamba Kitulo? Bila shaka umeyaona hapo juu; sasa hebu jifunze majina yake walau kwa uchache kupitia picha hapa chini:-

3. Maumbile

Kitu kingine kinachoifanya Kitulo iwe spesheli ni maumbile ya ardhi yake na miinuko inayoonekana ndani yake, uwepo wa vilele vyake virefu zaidi katika upande huu wa nyanda za juu kusini, ziwa lake la Kreta linalojulikana kama Dhambwe na mengineyo ni mojawapo ya mambo yanayoifanya Kitulo iwe sehemu spesheli.


-Lake Dhambwe

Ukiwa ndani ya hifadhi unaweza pia kutembelea mapango haya ya Mulivili ambayo waliyotumia mababu zetu kujificha wakati wa vita via makabila

Ukitazama hii video unaweza kuona namna gani Kitulo ni mahapa pema pa kutafakari uwezia wake Muumbaji.

4. Wanyama

Miaka ya hivi karibuni shirika letu la hifadhi za Taifa waliwarejesha wanyama waliotoweka hifadhini Kitulo kwa ushirika  na wadau wa maswala ya mazingira na viumbehai; wanyama kama Swala na Pundamilia waliletwa Kitulo kutokea hifadhi za Mikumi na Ruaha. Uwepo wa wanyama hawa pamoja na wanyama wengine wa asili vinafanya hifadhi hii iwe na thamani zaidi. Hifadhi inasema kuwa ukiwa Kitulo ni rahisi kuwaona wanyama wengine kama Duikers, Mbweha, Sungura, Mbega (Weupe na Weusi), Minde, Mbuzi Mawe na Rungwecebus Kipunji. Katika wanyama hao ukiacha Pundamilia na Swala ambao wanaonekana kwa urahisi.

Kwa bahati nzuri mimi binafsi nimeshuhudia wanyama aina ya Swala na Pundamilia wakiletwa hifadhini Kitulo, Shukrani kwa Ushirika la Utunzaji wa Wanyamapori la WCS (Wildlife Conservation Society) na mamlaka husika kwa kunipa kazi ya kurekodi video/picha za urejeshwaji wa wanyama hao katika hifadhi ya Kitulo kupitia kampuni yangu ya Studio Native (www.studionative.co.tz).

Unaweza kutazama video hizi za Zoo Transfer hapa chini

Kwahiyo, ukiwa kitulo huishii tu kufurahia mandhari, unaweza kuona Wanyama pia.

Tim Davenport  ambae ni muanzilishi wa shirika la WCS (Wildlife Conservation Society) lenye makao yake makuu huko Amerika aliwahi kunieleza kuwa hizi video za uhamishwaji wa wanyama kwenda Kitulo ambazo tulizitengeneza ndani ya hifadhi ya Kitulo, zilitajwa kuwa video bora za uhamishaji wa wanyama duniani kwa mwaka 2019.

Kongole kwetu 🙂 🙂

5. Ndege

Hifadhi ya taifa ya Kitulo ni sehemu muhimu duniani kwa makazi na mazalia ya ndege mbalimbali, wakiwemo ndege wakaazi na wageni kutoka Ulaya na nchi zingine za Afrika. Ndege huja kutokea makwao na kuzalia vifaranga vyao hifadhini Kitulo, kisha vikiisha kukomaa mbawa zao huruka hadi makwao huko Ulaya na Afrika.
Ukiwa hifadhini wanapatikana ndehe kama Korongo Mayobwe na Korongo Mweupe wanaotoka nje ya nchi, baadhi ya ndege wakaazi ni Kestrelli wadogo, ndege wawindaji, Njombe Cisticola, nk.

6. Maporomoko

Sehemu mojawapo inayovutia zaidi hifadhini Kitulo ni uwepo wa maporomoko mazuri mno katika ukanda huu wa kusini zaidi mwa Tanzania yetu. Ukiwa hifadhini pana maporomoko mengi lakini ninayoyapenda zaidi ni yale ya Mwakipembo na Nhumbe.

Maporomoko ya Mwakipembo yanapatikana jirani sana na geti la hifadhi, si marefu sana lakini yamewekewa nakshi nzuri kwa jailli ya Picnic.

Hapa ni mahali mahususi kwa ajili yako na mwenzako, katika matembezi yenu ya kila siku au katika siku yenu ya harusi, hapa panafaa pia iwapo utahitaji muda wako binafsi.

Maporomoko ya Mwakipembo Waterfalls

Maporomoko ya Nhumbe yapo walau kilomita 21 kutoka geti la hifadhi, haya ni mojawapo ya maporomoko marefu zaidi kusini mwa Tanzania ukiacha yale ya Kalambo.  Maporomoko ya Nhumbe yanataka kufanana na yale ya Malamba huko Rungwe, lakini kwa faida ya urefu wake na kuwemo ndani ya hifadhi iliyo juu zaidi; Nhumbe inabaki kuwa sehemu nzuri kwa ajili yako na wenzako.


Weka rekodi ya kuogelea katika pool ya Nhumbe Falls, lakini jiandae na baridi.


Picnic Area katika maporomoko ya Nhumbe

This is my best part of my stay in the park, wageni wangu hufurahishwa na mapumziko katika viota vilivyopo jirani na maporomoko, na lunch huwa nzuri sana ikiliwa hapa.


Wageni wangu kutoka umoja wa mabenki (Umoja Switch) katika hifadhi ya Kitulo

7. Malazi

Kama zilivyo sehemu zingine zozote za safari yako, mahala pazuri pa kulala ni sababu ya safari yako. Fikiria kupumzika hapa baada ya kuwaona Pundamilia, Maporomoko na Ndege.

Hifadhi ya Kitulo inazo Bandas nzuri za kulala kwa ajili yako na wenzako 🙂 🙂

Ukiwa hifadhini baasi jiachie…


Wageni wangu (Familia ya Kodtek) kutoka China


Wageni wangu kutoka Arusha wakifanya ‘fotoshuti’ ndani ya hifadhi


Asubuhi hifadhini, fanya unachotaka lakini usi-offroad 🙂 🙂

 


Unapenda picha? Backdrop na Maji ya mto Nhumbe hapo Nhumbe falls ni kiboko 🙂 :), tazama namna Julieth alivyotokelezea!!!

Mamlaka ya hifadhi Kitulo imejitahidi sana kuweka miundombinu sawa kwa ajili ya wageni wanaotembelea hifadhi hii, huenda some of the smaller SUVs kama Dualis, au Rav 4 zikaweza kuhimili sehemu nyingi ndani ya hifadhi. Ni muhimu sana utumie gari ukiwa ndani ya Kitulo ili uweze kuyafikia maeneo yake mengi yaliyotawanyika ndani yake.

Fahamu kuwa wakati wa mvua hasa hizi za masika, ni lazima utahitaji a serious 4×4 ili uweze kutembea vema kwa gari ndani ya hifadhi, ikiwemo hasa maporomoko ya Nhumbe ambako barabara yake huwa na changamoto wakati wa mvua nyingi.

Chakula: Kitulo huenda pasiwee na chakula ndani ya hifadhi, mara zote shauriana na mwenyeji wako ni namna gani utakula ukiwa hifadhini.

Viingilio: Mswahili mwenzangu au mkaazi wa Afrika Mashariki ni 5,900/- Tshs pekee, Non Residents ni USD 35.4, Expatriates ni USD 17.7

Malazi: 29,500/- kwa mswahili mwenzangu au mkaazi wa Afrika Mashariki, na USD 41.3 kwa Non Residents na Expatriates

Njia: Unaweza kufika Kitulo kwa kupitia Chimala au Isyonje

Makala hii imeandikwa na Shah Mjanja.

Shah Mjanja ni mpiga picha wa muda mrefu na muongoza wageni, Muandishi na Mtayarishaji wa makala za televisheni na filamu, Mhifadhi, Mwanamuziki na Msafiri. Ni muanzilishi wa Everyday Mbeya na Studio Native.

Shah Mjanja ni Ofisa wa Habari za klabu ya Mbeya City FC.

Tunawakaribisha wafanyabiashara na watoa huduma kufanya ushirika nasi kupitia kipindi chetu cha Utalii kinachoruka Jumamosi na Jumapili kupitia 100.9MHz redio Access FM. Kipindi chetu kinasikika mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Rukwa, Katavi, Songwe, Singida na Tabora.

Unaweza kushiriki nasi kama mdhamini.

Mawasiliano:

Ofisi: Posta House FL,
02 Posta Street, 53100 Mbeya
PO. Box 312 Mbeya

Simu: +255-682-326410
Barua Pepe: shah@everydaymbeya.com

ONYO: Picha zilizotumika katika makala haya zinamilikiwa kisheria na Studio Native na ni mali ya Studio Native, au/na washirika wake au za wamiliki wengine. Matumizi pasipo ruhusa au/na kwa lengo tofauti na mahudhui yaliyokusudiwa ni kinyume cha sheria na huenda ukawajibika.

Haya, basi sindikiza makala haya kwa kusikiliza kibao chao Marquiz kiitwacho Makumbele 🙂