Kiangazi kinakatika, lakini bado muda unapatikana kufurahia jua, kutokea Kawetere lilipo bonde la Ufa hadi maporomoko ya Kalambo.

Hello Everyday Mbeya, wasalaam!

Muda mrefu sijakuandikia makala zangu za upekuzi na nimefikiri kabla mvua hazijashamiri basi ni vema nikakupa madokezo machache yatakayokufanya uiage ‘summer’ kwa uzuuri.

Lakini kabla sijaendelea, ushawahi pata nafasi ya kutembelea hifadhi ya Kitulo?


Wageni wetu wakiwa hifadhini

Well, muda muafaka wa kwenda Kitulo umekaribia na ni miezi ya Disemba hadi Machi inayofanya hifadhi hii adhimu kuwa mahiri zaidi.
Kwa taarifa zaidi za kitalii kuhusu Kitulo usiache kufuatilia instagram yetu (@everydaymbeya).

So, kabla sijakuibia muda mwingi twende moja kwa moja katika manejo machache niliyoyachagua kwa ajili yako ili uweze kutembelea kabla kiangazi hakijaisha. Lakini kama vile haitoshi ninakuruhusu uwasiliane nami wakati wowote ukihitaji kufika maeneo haya

1. Isimila Stone Age

Selfi yangu juu ya ‘natural pillars’

Isimila Stone Age ni sehemu muhimu zaidi duniani ya kujifunzia mabadiliko ya tabia za binadamu wa kwanza kutokana na kupatikana kwa masalio mengi ya nyenzo alizotumia binadamu wa wakati huo. Nyenzo hizo muhimu zilimsaidia binadamu wa kwanza kuishi kwa unafuu na mazingira yake. Licha ya kwamba makumbusho rasmi ya Mtemi Mkwawa yapo mahala pengine, lakini ukiwa Isimila utapata faida ya kujifunza kuhusu mwamba huyu aliyezishinda vita nyingi, zipo mali na akiba tele katika mfumo halisi na ule wa machapisho vitakavyokusaidia wewe msafiri kujifunza habari za kale na watu wake.

Lakini kama haitoshi utaweza pia kutazama hizi natural pillars ndani ya Isimila. Hii ni milingoti ya asili iliyojivika nakshi za kuvutia, unapopita ndani yake utajihisi kama upo ndani ya sinema ya kihistoria miaka ya kale sana. Maumbile haya yametokana na mmomonyoko wa ardhi ‘overtime’.

Isimila ipo mkoa wa Iringa takribani kilomita 18 kutokea Ipogolo. Ukiwa Iringa usisahau kutembelea sehemu zingine kama hifadhi ya Ruaha, hoteli nzuri za Sunset na Royal pamoja na maeneo mengine. Mara ya mwisho nilipokua Iringa nilitembelea Coffee shop ya Asas na nikayajaribu Maziwa ya ngamia kwa shillings 2,000/- tu. Ukiwa Iringa utashangazwa na uhusishwaji mwingi wa Kitalii na maeneo yake muhimu kuanzia wageni, wenyeji, utamaduni wa shughuli za watu.

2. Mbozi Meteorite

Kimondo cha Mbozi si kitu kinachotajwa sana katika utalii hapa Tanzania lakini ni kivutio muhimu sana kwa elimu hasa inayohusu mambo ya anga. Katika vimondo 8 vilivyodondoka nchini Tanzania, kimondo cha Mbozi ni cha kwanza kwa ukubwa kikiwa na tani zaidi ya 12 na muonekano usiofanana na vimondo vingine duniani. Katika Afrika kimondo chetu ni cha pili kwa ukubwa.

Kimondo hiki cha Mbozi kinapatikana kilomita 70 kutoka Mbeya mjini kupitia barabara ya Zambia katika wilaya ya Mbozi ambayo sasa ipo mkoani Songwe.

Kimondo hiki kina mchanganyiko wa madini  ya chuma, shaba na nickel, kinabakia cha baridi wakati wote wa mwaka ikiwemo kipindi cha jua kali.

Ukitembelea Kimondo usisahau kwenda mpaka wa Tanzania na Zambia kutazama mji wa Tunduma ulio muhimu kwa Serikali na Taifa. Tunduma ni mojawapo ya mipaka muhimu zaidi kutokana na kuunganisha nchi nyingi zisizo na bahari kupitia watu na mizigo, lakini pia mji unaofuata upande wa Zambia uitwao Nakonde ni mojawapo ya miji muhimu sana kwa biashara na watu. Moja ya maduka yangu mashuhuri ni ZamBeef, hawa ni wataalamu sana wa bidhaa za nyama na maumbile yake kuanzia Kuku, Ngo’mbe, Maziwa, Mafuta na mengineyo.

Kila nikiwa ZamBeef naikumbuka Tanganyika Parkers pale Kawe, 🙂 🙂 🙂 .

Basi jumlisha ZamBeef na ubora wa thamani yetu ya shilingi, ni wazi ukienda Nakonde utarudi na kapu kubwa.


Mji wa Tunduma kutokea juu, unaweza kuona Tanzania na Zambia katika picha hii.

3. Great Rift-Valley View, Kawetere

Mimi ni mmojawapo ya watu wanaopenda kuendesha barabarani, tena wakati fulani bila sababu yoyote 🙂 🙂 🙂 , iwapo wewe ni mmojawapo basi mahala pa kufanya safari ni barabara ya kushangaza inaoyoelekea Kawetere, tena si mbali sana na mjini. Takribani kilomita 30 kutoka Mbeya mjini lipo eneo muhimu ambalo unaweza kutazama muonekano wa bonde la Ufa katika pande tatu, hii ni sehemu pekee duniani utaweza kutazama bonde hili kutokea Kusini, Mashariki na Magharibi.

Hakuna sehemu ingine duniani kote isipokua hapa.

Bonde la Ufa liliundwa miaka zaidi ya milioni 135 iliyokwisha kwenda na ni sehemu nzuri ya kuyatazama maumbile mazuri ya ardhi na milima yake. Ukiwa hapa utatazama eneo chepe la ihefu na kilimo chake cha mpunga huko wilayani Mbarali, lakini utaona pia milima ya Uporoto lilipo ziwa Ngosi na safu za milima ya Mbeya. Ukiwa na macho mazuri unaweza kuona hadi hifadhi ya Ruaha, wajuzi wanasema hili lilikua lango la kwenda hifadhi hiyo siku za kale.


Uumbaji wa Mwenyezi Mungu hauachi kushangaza, tazama barabara ya kwenda Chunya ilivyo nzuri kutokea juu.

Huku ndipo ilipo barabara iliyo juu zaidi Tanzania.

Ipo park ya wazi kwa ajili yako na rafiki zako. Siku za wikendi mimi na jamaa zangu huenda eneo hilo kutazama tena na tena bonde la Ufa, mandhari za barabara na uzuri wa nchi. Wakati wa usiku eneo hili hupendezeshwa na mataa ya nchi yanayowaka katika majumba huko chini, lakini pia machweo ya jua katika milima ya Mbeya ni mojawapo ya sababu tele za kwenda huko.

Eneo hili pia linafaa kwa ajili ya party za makundi machache hadi mengi.


Huyu hapa ni Ruga, Ditto, Mwasiti na Kennedy the Remmedy katika bonde hilo la Kawetere wakati wa shughuli rasmi za Everyday Mbeya na washirika wake.

Kutoka Kawetere hadi mji wa Chunya ni kilomita arobaini tu, hivyo ukiwa na tanki la ziada unaweza kanyaga mafuta hadi Chunya mjini ukajionee mji wa dhahabu unavyong’arishwa na wachimba madini.

4. Kalambo Falls

Ni mastaajabu ya Mwenyezi katika mpaka wetu na ule wa Zambia yanapopatikana maporomoko haya yakustaajabisha. Hii ni Kalambo Falls inayopatikana takribani kilomita 140 kutokea mji wa Sumbawanga. Maporomoko haya yana urefu wa mita 235 na upekee wake wa anguko moja yanayafanya yawe ya kwanza Afrika licha ya kuwa yanasemwa kuwa ya pili Afrika baada ya yale ya Tughela yaliyopo huko Afrika kusini.

Maporomoko ya Kalambo yapo mkoani Rukwa katika wilaya ya Sumbawanga mjini, kutokea Mbeya ni takribani kilomita 350 hadi Sumbawanga.

Maji ya mto Kalambo yanaligawa Taifa letu na Zambia, yanavyodondoka yanaifanya Kalambo iwe bora zaidi ya maporomoko yote duniani. Mto Kalambo unasafiri kutokea hapa hadi ziwa Tanganyika, ziwa lenye kina kirefu zaidi Afrika yote.

Kutokea Kalambo hadi kijiji cha Kasanga lilipo ziwa Tanganyika ni wastani wa kilomita 5 tu, na hapo ndipo mahala penye machweo bomba zaidi nyanda za juu kusini. Ukiwa Kalambo au Ziwa Tanganyika ni jirani sana kwenda hifadhi ya Taifa ya Katavi au ziwa Rukwa.

Machweo ziwa Tanganyika, Kasanga

Muonekano wa ziwa Tanganyika wakati wa asubuhi

5. Mbeya Region

Mbeya ni mkoa ulio kusini zaidi mwa Tanzania na kwa upekee una maeneo mazuri ambayo unaweza kuyatembelea wakati huu kabla mvua hazijaanza kunyesha kwa kasi. Haya hapa ni maeneo ambayo nakushauri uyatembelee  🙂


Mlima Mbeya, kilele 2826m juu ya usawa wa bahari


Mashamba ya Chai Rungwe

Soko Matola, mji mkongwe ilipo nyumba aliyoishi Mwl. Nyerere

Ifisi Zoo and Ravine, Mbalizi

501 Garden, Meta

Mashamba ya Mpunga, Kapunga Chimala

City Centre, Mbeya

Wasalaam,

Makala hii imeandikwa na Shah Mjanja.

Shah Mjanja ni mpiga picha wa muda mrefu, Muandishi na Mtayarishaji wa makala za televisheni na filamu, Mhifadhi, Mwanamuziki na Msafiri. Ni muanzilishi wa Everyday Mbeya na Studio Native.

Shah Mjanja ni Ofisa wa Habari za klabu ya Mbeya City FC.

Mawasiliano:

Simu: +255-682-326410
Barua Pepe: shah@everydaymbeya.com

Kama kawaida yetu, nakuachia wimbo wa ‘Mtoto Kaanza Tambaa’ wake King Kiki, miaka ya 2008 – 2011 Mzee alikua akiimba katika ukumbi mmoja pale Ubungo, basi mimi na jamaa zangu tulikua tukihudhuria sana bendi ya Kiki siku za ijumaa na wakati fulani mida mibovu baadhi ya wapigaji wake walituachia vyombo nasi tupige, nakumbuka nilikua na mwanangu anaitwa Mashindano Livinus a.ka. King DD, yeye alikua anashika microphone mimi nakaa Mwenyekiti kinanda. Hatari!

It was fun 🙂

Enjoy!