Ndege zisizo na rubani zimechagiza sana Utalii… Kila sehemu iliyooneshwa kwa picha za juu inavutia, lakini pia inashangaza; kwa sabbau macho yetu yanapata kuona eneo husika kwa kutumia jicho la ndege (drone) na kupata muonekano ambao hatuwezi kuona kila siku.

Ninakueletea makala inayoangazia drone na Tehama zake.

Hivi karibuni mamlaka za Anga wameleta utaratibu mpya unaozitaka drone zote nchini zisajiliwe. Utaratibu huu mpya umepokelewa tofauti na watumiaji wengi wa drone, wadau na watanzania wa kawaida. Fahamu kuwa utaratibu wa kusajili drone umekuwepo toka zamani na dunia yote katika kila Taifa umewekwa utaratibu kuhusu usimamizi wa matumizi ya drone, mojawapo ikiwa ni kusajili drone yako na mrusha drone husika. Fahamu kuwa drone hizi ni hatari kwa usalama wa ndege zetu mfano za ATCL na kadhalika, na ni hatari sana kwa usalama wa watu au kwa makosa mengine ikiwemo jinai.


Drone ikiruka juu ya Ziwa Ngosi, Mbeya.

Drone zina uwezo mkubwa mfano modeli ya DJI ya Mavic Pro inaweza kuruka hadi kilomita 3.5 juu na kwenda mbele hadi kilomita 7.8. Kwa sababu hii, drone imesaidia sana upatikanaji wa picha nyingi za mandhari, utafiti na kusaidia katika maeneo mengine yakiwemo msaada wa dharura, uokoaji na huduma mashambani. Ni lazima tukubali pia drone imesaidia sana katika sekta ya utalii na safari, hata hapa nchini kwetu Tanzania kupitia picha za drones maeneo mengi yameonekana kwa ubora zaidi.

Hapo badae nitaeleza lini makatazo haya yalianza na kwanini utaratibu huu uliletwa na baadae kusisitizwa zaidi. Nitaonesha pia nchi zingine ambazo zimeweka sharia katika kusimamia matumizi ya hızı drone.


Picha hii nimepiga kwa drone juu ya Ziwa Nyasa, Kyela Mbeya.

Fahamu kuwa adui mkubwa wa ndege zenye rubani ni Birds Strike, drone na hali ya uwanja. Huko nyuma Fastjet iliwahi kukutana na shambulio la ndege (birds strike) hapo JKIA na ikasitisha safari yake. Fahamu kuwa hali uwanja (airstrip) pia ni hatari kwa ndege zetu. Mfano hizi Airbus zetu mpya sijaona zikitua kule Songwe Iinternational Airport huko Mbeya na huenda ni kwa sababu ya ubora wa njia yake ya kushukia ndege.

Ukiondoa birds strike na ubora wa uwanja, drone zinaweza kuwa hatari sana kwa ndege zenye rubani ukiacha sababu nyingine zikiwemo usafirishaji wa dawa ya kulevya au silaha kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kadhalika. Fahamu kuwa drone inaweza kubeba hadi kilo tatu. Baadae nitaeleza kuhusu elimu ya drones kwa kiasi na ni bahati mbaya elimu hii ni ngeni kwa watu wengi wakiwemo watu wa aviation wenyewe na kwa aibu zaidi hata kwa watumiaji drone wenyewe.

Hapa pichani ni mimi na rubani wa ndege hii ndogo iliyosajiliwa huko Malawi, picha hii niliipiga kwa drone wakati ambao nilikuwa uwanja wa ndege katika shughuli rasmi nilizopewa na mamlaka ya viwanja vya ndege Tanzania. Wakati tunajipiga picha hii kwa drone iliyokua hewani, nilikua nikimpa maarifa rubani huyu kuhusu elimu ya drone ambayo yeye binafsi alikua haelewi chochote kwa wakati huo.

Fahamu kuwa bila Kigali hupaswi kurusha drone katika viwanja vya ndege.

Drone haipaswi kuruka zaidi ya mita 500 juu ya usawa wa Bahari. Huo ni usawa ambao ndege zenye rubani huruka. Mfano ukiwa Ifisi Hotel au pale Rafine Zoo jijini Mbeya au hapo Dar ukiwa Kipunguni au Jet Lumo na ukirusha drone yako juu zaidi ya mita 500, unayo hatari ya kukutana na ndege na mkapata ajali.

Ndio maana drone hazipaswi kuruka zaidi ya mita 500 juu ya usawa wa bahari. Lakini drone hazipaswi kabisa kuruka jirani na viwanja vya ndege kwa wastani wa kilomita kama 2 hivi (sina hakika na hii perimeter) kutoka uwanja wa ndege. Ukinunua drone yako utakuta ina masharti haya ambayo yanawezeshwa na GPS (Global Positioning System) iliyomo ndani ya drone yako. Lakini, haya yote yanawezekana kwa GPS na ndio maana ni muhimu mrusha drone ahakikishe drone yake imeshika GPS ili iweze kutambua kuwa hapa ni uwanja wa ndege au sehemu ingine usipopaswa kuruka.

GPS ni muhimu sana kwa mambo ya anga yote na katika drone ukiwa katika GPS mode basi drone huwa na ufanisi wa asilimia 100. Sasa kama ndege mfano kunguru alisababisha hitilafu ya injini ya ndege, itakuaje drone yenye vyuma ikiingia katika injini hiyo?

Hapo ndipo makatazo yanapoanzia. Sasa kama drone zina GPS kwanini wanaweka tahadhari na usimamizi?

Katika soko la kawaida (watumiaji) kampuni mashuhuri inayounda drone nyingi ni ya kichina na inaitwa DJI. Zipo kampuni zingine tele lakini hawa DJI katika drones na vifaa vya picha unaweza wafananisha na Toyota tu. Wana aina nyingi sana za bidhaa zao ikiwemo drones. Fahamu kuwa GPS haipatikani maeneo yote vizuri, mfano tu ukiwa chumbani kwako au nje ya mji GPS huwa haiko imara. Kwahiyo, GPS huwa imara sana sehemu yenye minara mingi ya simu au shughuli nyingi za electronics. Kwa kutambua hili watengenezaji wa drone huzipa drones zao mode za aina kama tatu ili ziruke. Mojawapo ni GPS mode na zingine ni Attitude mode na Positioning Mode.

Drone nyingi zina hizi mode zote na hapo ndipo hatari ya anga inapoanzia. Ukiwa sehemu ambayo haina GPS drone itatumia hizo mode zingine lakini kwa tahadhari watengenezaji wa drone wamezuia mode mojawapo isiruhusu drone kuruka zaidi ya mita 30. Hili ni angalizo ili usiweze kuruka sehemu ambayo haziruhusiwi mfano zaidi ya mita 500 juu ya usawa wa bahari au jirani na viwanja vya ndege katika eneo ambao ndege inaweza kuwa inapita.

Lakini, ukiwa katika Positioning mode, mimi ninaweza kwenda hadi kilomita 3 juu kulingana na uwezo wa drone husika. Sasa nikiwa Mbalizi hapa Mbeya ni dhahiri shahiri taenda kugongana na Bombardier yetu iliyo jirani kutua uwanjani Songwe. Nani anataka kupoteza Bombardier zetu kirahisi hivi? Kwahiyo kila nchi au ukanda una sheria zinazosimamia matumizi ya drones.

Mara zote watengenezaji wa drone wanasisitiza kutokurusha drone nje ya line of sight (mstari wa muonekano kati yako na drone). Ni rahisi sana kuimudu drone yako katika mazingira ambayo unaiona, hii husaidia usigonge kitu kingine au kupoteza drone yako. Lakini kwa warusha drone mtafahamu kuwa yapo mazingira huwa tunarusha hadi nje ya upeo wa macho hasa tunapohitaji picha kubwa zaidi. Mfano wakati napiga picha ya ziwa Ngosi huko Mbeya, ilinilazimu kuruka juu mita 500 na kisha kurudi nyuma kilomita 2.5 ili nipate picha halisi ya ziwa. Huu ni umbali ambao macho hayawezi kuona. Wakati kama huu utategemea remote controller kuiongoza ndege yako na kupata taarifa za kifaa chako kilichopo angani.


Ziwa Ngosi (2.5km Upana na 1.6km Urefu)

Fahamu kuwa drone huongozwa na controller ambayo hukupa taarifa muhimu kama dashboard ya gari yako. Itakuonesha uwezo za betri, speed ya ndege yako na kasi ya mabawa yake, itakuonesha umbali ilipo juu na mbele/nyuma lakini pia itakuonesha hali ya hewa kama upepo na mengineyo.

Nchi nyingi zina chombo kinachosimamia mambo ya anga mfano America wana FAA, Sweden wana TAS na hapa kwetu tuna TCAA inayosimamia maswala haya. Hapa nchini sheria za drone zipo huu mwaka wanne isipokua hazikuwa zinazingatiwa sana. Na ni lazima mteja akitaka fulani amrushie drone mfano katika harusi yake, atapaswa amuulize mrushaji una kibali?

Miaka kenda zamani nilipata kandarasi toka Nairobi, ambapo agency moja ya Kenya inayotengeneza film za Bill & Melinda Gates Foundation ilihitaji huduma zangu za drone katika film zao. Swali la kwanza, tutumie certification zako za drone!

Kwa wakati huo sikua na Certification na awali walikataa lakini producer wao moja alivutiwa sana na shots zangu, akasema tunakupa kazi, tunahitaji shots, risky ya usalama itakua juu yako. Maana yake ni kuwa nili-kiuka masharti kitu ambacho wengi tunafanya. Kwa huko Ulaya hizi sharia zinazuia mengi isipokua urushaji wa drone nyumbani kwako, ndani ya ukumbi wako au kijijini kabisa ambako ndege hazipiti.

Sharia hizi ni muhimu sana.

Hata kwako wewe, fikiria uko unaoga kwa choo chako cha wazi hapo uani, au upo na kimwana mnaogelea huko Bhujonde ziwani Nyasa. Kisha ghafla Mjanja huyo anakuja na drone na kukurekodi, uhuru wako unakua mashakani.
Fahamu kuwa kila mtu anayo haki ya faragha.

Hii video ilileta sana taharuki baada ya kijana moja kurusha drone jirani kabisa na hii A380. Je, unafahamu Airbus A380 inapakia abiria wangapi? Fikiria watu wote hao wawe matatani kwa drone moja ya usd 800! Hizi ni sababu ambazo zinazuia na kuleta utaratibu wa sharia zinazosimamia matumizi ya drone.

Siku moja mimi na jamaa yangu tulipata dili tukachunguze kwa siri kwa kutumia drone gari iliyoibiwa na kufichwa ndani ya nyumba ya mtu. Tulikataa lile dili ingawa lilikua nono sana. Pia, mimi binafsi nimesaidia kufanya doria pamoja na wakala wa huduma za misitu huko mlima Rungwe kukagua maharamia wa mbao kwa kutumia drone au wakati mwingine kuchunguza dalili na chanzo cha moto misituni.

Hifadhi asilia ya mlima Rungwe Mbeya, hii ndio sehemu inayopokea mvua nyingi kuliko zote nchini.

Sasa fikiria, ukiwa huna kibali, au cheti, itakuaje? Kwahiyo, lazima uwepo utaratibu wa usimamizi wa matumizi ya drone. Maana kwa kujua ama kutokujua warusha drone wengi tumefanya makosa. Vipo viwanja vya ndege nchini ambavyo ni vipya na kwenye GPS havionekani. Maana yake ni kuwa ukienda pale unaweza kurusha drone. Sasa, kila mara warusha drone wanarusha drone zao mitaani, mfano wanakwaya wanarekodi video au maharusi wanasherehekea na wanatumia drone. Si ajabu ukakuta mtu anarusha drone muda ambao ndege inaruka kitu ambacho kinaweza kuleta ajali na madhara yakawa mabaya sana.

Lakini ukiwa mtaalamu na mvunja sharia, unaweza kudanganya na ukarusha drone katika maeneo ambayo drone kwa asili haipaswi kuruka mfano katika viwanja vya ndege. Awali nilieleza zile mode mbili katika operation za drone, maana yake ni kuwa ukiwa katika zile mode unaweza kurusha drone hata katika viwanja vya ndege. Pia, wako watumiaji wa drone ambao wame-uingilia mfumo wa uendeshaji na usimamizi wa drone zao kinyume na sera au mpangililio uliotoka kiwandani. Hawa wanaweza kurusha drone sehemu yoyote kitu ambacho ni hatari sana kwa usalama.

Mbali na hayo pia yapo madhara binafsi. Mfano wakati fulani mdogo wake na binti yangu nilienda naye field kumbe wakati wote alikua ananitazama, basi wakati naenda kula nikamuachia drone, Yeye bila ruhusa yangu akaiwasha akairusha juu na kisha wakati wa kushusha akashindwa, akaogopa, akaenda kuikamata na mikono. Akakata sehemu ya kidole. Fahamu kuwa panga za drone zina uwezo wa kumkata ndege na kumgawanya mara nne ndani ya robo sekunde.

Sasa turejee katika gharama za usajili wa drone maana hili ndilo eneo lenye ukakasi zaidi! Kwanza, gharama za kupata kibali zinataja fedha ambayo ni usd 100, lakini hazielezi mtihani au usaili wa kufaulu kurusha drone. Nilitaraji kama ambavyo nimeonesha madhara ya drone huko juu basi sharia ya usimamizi wa usajili wa drone ingehusisha pia mafunzo na mtihani wa ufaulu, kama ambavyo dereva anapaswa kuwa na leseni basi gharama tajwa ingekua ya kukizi mafunzo pia. Huko nje, wenzetu wana utaratibu wa usaili ili uruhusiwe kurusha drone na ni kitu kinachoshangaza kwa hapa nchini hakuna mtihani.

 

Je, Gharama za hiki kibali ni za nini? Je, ni kodi ya mapato au ni ada ya ushiriki wa anga? Je, kwa studio inayofanya biashara na kulipa mapato TRA nayo itapaswa ilipie usd 100 za drone? Haya ni maeneo ambayo huenda yalihitaji muda kuyatafakari. Gharama ya usd 100 kwa urahisi tuifananishe tu na 220,000/ Tshs. Ada hii ni ya mwaka na utapaswa uihuishe kila baada ya miezi 12. Drone hizi ambazo tunaziona sana katika shughuli zinaweza kuwa zinauzwa kati ya usd 800 hadi 1500, ni drone zinazotumiwa na watumiaji wa kati.

Watu wengi sana wakiwemo wadau husika walilalamikia ada za Kigali cha kutumia drone, malalamiko menage ni ukubwa wa gharama husika. Kwa hesabu rahisi kima cha chini cha kukodi drone kwa siku hakiwezi pungua 150,000/- Tshs, sasa fikiria huyu mtu mwenye drone kwa mwezi atarusha drone mara ngapi? Tuchukulie kuwa kila wiki atarusha drone mara moja, maana yake kwa mwezi ataingiza 600,000/-, na kwa mwaka ataingiza 7,200,000/- Tshs. Katika hiyo fedha ukitoa asilimia 30 ya gharama za uendeshaji ikiwemo ununuzi wa betri iwapo ina hitilafu, usafiri na matumizi mengine ni wazi mtumiaji wa drone atabakiwa na kiasi kikubwa.
Kwahiyo, kwangu mimi binafsi bado naona ada ya usd 100 ni stahiki na haiwezi kumuumiza mtumiaji wa drone.


Wakati naandika makala hii, TCAA/TCRA haikuwa imeweka mafunzo kwa warusha drone, tunayo furaha kwa sasa mafunzo yanatolewa licha ya kuwa tozo za mafunzo ni kitendaliwi. Mtumiaji wa drone mojawapo alisema ‘zile ada za mafunzo kwa vyovyote zilivyokusudiwa hazina uhalisia’

Swali langu kwa mamlaka, kwanini wanatumia usd badala ya shilingi? Zifuatazo ni sehemu ya picha na video zangu za drone.


Sunset ya Ziwa Tanganyika, Rukwa

Maporomoko ya Kalambo, Rukwa.


Fukwe za Matema na milima ya Livingstone, Kyela Mbeya


Jangwani, Dar es Salaam
Maporomoko ya nhumbe, Kitulo Mbeya.


Uwanja wa Taifa (B. W. Mkapa)


Maporomoko ya Kaporogwe, Mbeya


Kapunga Rice Farm Project Limited, Mbeya


Mashamba ya Mpunga, Kyela Mbeya

Makutano ya Mafiati, Mbeya


Bonde la Ufa, Kawetere Mbeya

Wasalaam,

Makala hii imeandikwa na Shah Mjanja.

Shah Mjanja ni mpiga picha wa muda mrefu, Muandishi na Mtayarishaji wa makala za televisheni na filamu, Mhifadhi, Mwanamuziki na Msafiri. Ni muanzilishi wa Everyday Mbeya na Studio Native.

Shah Mjanja ni Ofisa wa Habari za klabu ya Mbeya City FC.

Mawasiliano:

Simu: +255-682-326410
Barua Pepe: shah@everydaymbeya.com

 

Kama kawaida yetu, nakuachia wimbo wa Msongo Ngoma ‘Cheusi Mangala’ ukuliwaze baada ya kusoma makala haya.