Hello Adventure!

Some day-break stories!

Wapi jirani naweza kwenda? Leo nawaletea sehemu chache ambazo unaweza kwenda nje ya Mbeya na kufurahia upekuzi wako. Nitaanza na Isimila Stone Age Site. Hifadhi hii adhimu ipo eneo la Isimila nje kidogo tu ya mji wa Iringa. Shukrani sana kwa rafiki yangu Sisco ambaye ni muongozaji wa watalii hifadhini Isimila, yeye amenisaidia sana mimi na wenzangu tulipofika mahala hapo na hata kuandika makala haya.

Isimila stone age site ni sehemu muhimu duniani ambayo historia ya kale inapatikana, mahala pale pana shuhuda kuhusu matumizi ya mawe kwa binadamu wa enzi hizo na dunia inaitambua Isimila kama ‘the most important archaelogical sites’.

Selfi juu ya korongo lenye natural pillars

Katika hifadhi hii pana mikusanyo ya nyenzo za mawe za kale na maumbile ya ardhi yaliyotokana na kuhama kwa mchanga na maumbile yaliyoumbwa na maji.

Binadamu wa kale alitumia nyenzo kurahisisha maisha na nyenzo hizo zinaonekana hapa Isimila, zipo aina mbalimbali za mawe zilizochongwa ama kubondwa na kutumika kama nyundo, mshale, kikwaruzio na zingine.

Hifadhi hii ya malikale ipo jirani tu na mji wa Iringa takribani kilomita 15 kutokea Iringa mjini na ukifika Isimila utalipia @2000/- Tshs kwa mswahilil mwenzangu au mkaazi wa Afrika Mashariki ili kuingia hifadhini. Ukitaka guide itakugharimu shilingi elfu kumi ya zaidi na ni muhimu uranie utalii kwa msaada wa guide ili uweze kupata elimu zaidi ya Isimila.

Serikali kwa kutambua umuhimu wa Isimila iliamua kuiweka hifadhi hii chini ya usimamizi wa hifadhi ya Taifa Ruaha. Fahamu kuwa hifadhi hii haipokei fedha mkononi hivyo itakulazimu uwe na akiba katika simu yako au kadi ya kibenki kufanya malipo.

Isimila ipo korongoni katika nyika za Iringa, na kwa miaka tele inathaminiwa kama eneo la kimataifa la kujifunzia mgawanyiko mkubwa wa tabia na mabadiliko ya kibinadamu.

Sehemu nyingine muhimu hapa Isimila ni ‘natural pillars’, nguzo hizi za asili zimetokana na mmomonyoko wa Udongo uliosababisha kutokea kwa nguzo hizi. Hizi natural pillars zinaipa Isimila muonekano maridhawa na zimekua kivutio kwa watembezi wengi.

Uzuri wa hifadhi hii ni kuwa hutohitaji gari kufanya utalii wake bali utatembea kwa miguu na kujionea uzuri wake unaotokana na hisoria ya kale ikiwemo nyenzo za mababu zetu na nguzo za asili.

Sasa, nini maana ya neno Isimila?

 Wakati wa vita kuna baadhi ya askari wa Mkwawa walikimbia vitani na kwenda kujificha maeneo ya mbali, sasa alikuwepo askari moja aliyeitwa Mwautenga. Alikua ni askari muhimu na alitafutwa sana, hapo baadae ikaonekana Bwana Mwautenga alijificha huko ambako sasa tunapaita Isimila. Sasa kwa kabila la wakaazi wa huko walisema Pepisimike, wakimaanisha amejificha hapa.

Neno pepisimike ni nano la Kihehe ambalo lina-maanisha mahala ambako mtu amehamia na hana mpango wa kurudi alipotoka (alipojisimika). Kwa kiswahili cha mjini cha sasa tungesema alipojichimbia!!!

Sasa wageni hawakuweza kutamka Pepisimike, wakauma-uma maneno hadi kutohoa neno ISIMILA. [Pepisimike-Isimike-Isimila]

Hifadhini hapa pana makumbusho ya silaha za jadi alizotumia Mkwawa, na nyenzo kibao walizotumia mashemeji zangu Wahehe na wabena kupikia, kulimia na mengine mengi.

Unahitaji kwenda Isimila? Wasiliana nasi

Unajua maana ya neno Mkwawa?

Mkwawa ni neno la Kihehe lililotokana na neno Mukwavinyika lenye maana ya mtu aliyezishinda tawala nyingi. Fahamu kuwa Chief Mkwawa aliwapiga mno wajerumani katika vita huko Lugalo tarehe 17 August 1891.

Nani kama Mkwawa? Mkwawa anaweza kuwa Chief Msaidizi Nduna Luwafu Songea Mbano, tazama makala yangu hapa chini inayoitwa Majirani Songea ujifunze zaidi kuhusu huyu Mbabe wa Ruvuma.

 

Wasalaam,

Makala hii imeandikwa na Shah Mjanja.

Shah Mjanja ni mpiga picha wa muda mrefu, Muandishi na Mtayarishaji wa makala za televisheni na filamu, Mhifadhi, Mwanamuziki na Msafiri. Ni muanzilishi wa Everyday Mbeya na Studio Native.

Shah Mjanja ni Ofisa wa Habari za klabu ya Mbeya City FC.

Mawasiliano:

Simu: +255-682-326410
Barua Pepe: shah@everydaymbeya.com

Kama kawaida, msikilize Vitali Maembe na kibao chake ‘Hamia Ndege’ kusindikizia makala haya.