KWA muda mrefu nimebishana na rafiki zangu wa Urithi Tours juu ya maporomoko yenye kuvutia zaidi. Nilishikilia msimamo wangu ya kwamba, hakuna maporomoko barani Afrika yenye kuvutia kushinda Victoria Falls kutoka Mto Zambezi kwenye mpaka wa Zambia na Zimbabwe. Nilishikilia msimamo wangu kwa muda mrefu kwa sababu nimekwenda Victoria Falls mara nyingi . Hivyo, nilikuwa najua ninachobishania.
Jambo ambalo sikuwa nalifahamu ni kwamba, sikuwa naifahamu Kalambo.
Kimsingi, sikuwahi kusikia kuhusu Kalambo Falls hadi mwaka 2017. Siku moja niliposhuka uwanja wa ndege wa Songwe jijini Mbeya, niliona bango kubwa likiyanadi maporomoko hayo. Lakini, sikuyatilia maanani sana. Niliendelea kuamini, taswira ya maporomoko ya Victoria ni yenye kuvutia zaidi. Kwa sababu, nimekuwa nikienda karibia kila mwaka.
Nilikosea.
Baada ya ubishani mkubwa na Urithi Tours, Februari 12 niliwasili Sumbawanga, mkoani Rukwa. Mimi nimekulia mji wa Tunduma mkoani Songwe. Lakini, sikuwahi hata mara moja kuwaza kufika Sumbawanga. Niliamini ni mji usiovutia. Nilikosea. Nilijithibitishia makosa ya mtazamo wangu mara tu nilipowasili Sumbawanga. Nilistaajabu kuona mji uliopangika vema, ukiwa na barabara zenye kuvutia.
Hata nilipowasili Sumbawanga, nilishikilia msimamo wangu kuwa Kalambo haitokuwa yenye kuvutia kiwango cha Victoria Falls. Nilionesha hata ushahidi wa maandiko mengi mtandaoni yanayoinadi Victoria Falls. Kwa kuwa Kalambo Falls haijulikani sana, niliamini haiwezi kuwa yenye kuvutia hata kidogo. Nikasema, si tutakwenda tukaone? Siku hiyo, na kesho yake, nikatumia kuizuru hasa Sumbawanga. Haikuacha kunishangaza. Ni mji mzuri sana. Nisisahau kukwambia, kuna mahindi ya kuchoma matamu kuliko pahala pengine popote.
Februari 14, saa 2.20 asubuhi, mimi na timu ya Urithi Tours tulianza safari ya kwenda Kalambo Falls. Nilivutiwa na uzuri wa barabara. Barabara hiyo inayokwenda bandari mpya ya Kasanga kwenye Ziwa Tanganyika (nitaandika kwa kirefu juu ya ziwa hili) imejengwa kwa kiwango cha lami. Hali ya hewa ilisisimua vilivyo.
Baada ya safari ya kilometa sabini hivi, tulichepuka kushoto kuishika barabara ya changarawe kwa kilometa zingine zipatazo kumi na sita. Safari kwenye mbuga ilisisimua sana. Nilifurahi kuona vijiji kadhaa njiani.
Wakati tunakaribia, niliona mawingu fulani yakiwa yamekusanyika mahali pamoja. Mwongozaji akaniambia ni mvuke wa Kalambo Falls. Nilitoa macho na kuutawanya mdomo wangu kwa mshangao.
Mawingu yaliyonishangaza.
“Haiwezekani!” nilisema.
Fikiria mwenyewe, uzuri huu upo Tanzania.
Sikuamini. Si kwamba, eti sikuamini kuwa kile nilichodhani ni mawingu ni mvuke wa maporomoko. La. Nimeona taswira hiyo mara nyingi Victoria Falls. Sikuamini kwamba, ninachokiona kimo ndani ya nchi yangu, Tanzania.
Tulikwenda hadi mahali tulipotakiwa kupaki gari letu. Bado niliendelea kuiona ile taswira ya mvuke ikitiwa nakshi na mwonekano wa uoto wa asili mlimani. Tulipopaki gari, tulishuka ngazi 117. Wakati tunamaliza, nilihisi kupata wazimu. Wazimu wa furaha. Mbele yangu, niliona gema kubwa ambalo upeo wa macho haukuweza kufika chini. Ule mvuke ambao sasa niliuona kwa karibu ulinisisimua mno. Niliyaona maji ya mto yakiporomoka chini ya ukingo mkali. Nilistaajabishwa na namna maji ya mto yalivyozunguka kidogo kurudi yalipotoka kabla ya kuanza kuporomoka. Wewe, umewahi kuona maji ya mto yakirudi yatokako? Nikaambiwa, ukingo wa upande mwingine wa mto, ni Jamhuri ya Zambia.
Sikuwahi kukiona kitu kizuri kama taswira mbele yangu. Nikawaambia wenzangu, “Victoria Falls ikasome upya boarding school ifanye na NECTA, ifeli halafu i-resit.”
Nikayaona kutokea juu pembezoni mwa Mto Kalambo.
Wakati mimi nikidhani ndiyo nimemaliza kuona maporomoko, wenyeji wangu wakaniambia hilo ni trela tu. Tukafanya hiking kuupandisha mlima kulia kwetu. Badala ya akili yangu kufikiria kimlima mbele yetu, iliendelea kuleweshwa na taswira kushoto kwangu. Kila nilipopiga hatua kwenda juu, ndivyo macho yangu yalivyoona zaidi uzuri wa maporomoko hayo na gema kubwa kabisa. Nikwambie tu, maporomoko ya Kalambo yana urefu wa mita 235. Maana yake, ni marefu kwenda chini kushinda Victoria Falls, yenye urefu wa mita 108. Nakwambia hivi, Kalambo ni ndefu mara mbili na zaidi ya Victoria Falls. Niamini mimi.
Tulipofika juu ya mlima tulioupandisha, nilizidi kuchanganyikiwa. Mbele yangu niliona safu za milima iliyojazwa kwa uoto wa asili wenye kijani iliyokoa, huku ukifunikwa na mawingu mepesi yenye kutia ladha mwonekano. Nikaziona ngazi ndefu na nyingi kushuka chini. Niliwauliza wenyeji idadi ya ngazi. Haikuwa ikijulikana. Nikawaambia, mbinu ya nzuri ni kutohesabu wakati wa kushuka, bali, wakati wa kupanda. Kama ulikuwa hujui, nakujuza sasa; mbinu hii inasaidia sana kutochoka wakati wa kupandisha ngazi. Akili yako inazama kuzingatia mahesabu badala ya zoezi kubwa la kupanda.
Ngazi kushuka chini kabisa mtoni.
Kila tunaposhuka, taswira ilizidi kunivuruga. Nilijikuta nikisema, “Wow, wow, wow, wow, woooow!” mithili ya king’ora cha gari la wagonjwa kwenye foleni ya Magomeni.
Msisimko wakati wa kushuka ngazi.
Niliyaona maporomoko mbele yangu.
Kalambo Falls.
Upande wa kulia chini ya gema nilishangaa kuona mimea ikitetemeka. Nilitazama kwa muda mrefu nikijiuliza kwa nini inatetemeka kiasi cha kutoa taswira ya mimea inayotembea? Baada ya kukosa jibu, nilimwuliza mwenyeji wangu. Akanijibu mtetemo unasababishwa na kishindo cha maporomoko.
Nikabaki, wooooooow!
Kila nikishuka, nilizidi kusisimka. Ule mvuke wa maporomoko haukishia tu kutoa taswira ya mawingu juu yangu, pali kunipa matone yenye kunifanya kutamani kushuka zaidi na zaidi. Wakati wenzetu Zambia na Zimbabwe wakiuita mvuke huo, Mosi-oa-Tunya, wakimaanisha, The Smoke That Thunders, sijalisikia jina la mvuke huo wa Kalambo.
Ooooh, Tanzania
Wakati tukipandisha kurudi, ndipo nilipozihesabu ngazi, nikishirikiana na wenzangu. Kuna ngazi za chini kabisa za zamani (zilizobomokabomoka) zipatazo arobaini na kitu. Lakini, kuna ngazi mpya kabisa 775 (ninamaanisha, mia saba sabini na tano).
Kama nilivyosema awali, kupandisha haikuwa kazi ya kuchosha hata kidogo kwa sababu tulikuwa tunahesabu ngazi. Umekuwa uzoefu wangu bora kuhusiana na nchi yangu Tanzania.
Mtu anaweza niuliza, kwa nini kwenye simulizi yangu hii nimekuwa nikitajataja Victoria Falls?
Kwa sababu, imetangazwa sana kiasi cha kujulikana mno. Ukienda Victoria Falls, hakuna siku utakuwa peke yako na wenyeji wako. Ni msururu wa watalii wakienda na kurudi, huku na kule. Kule Kalambo, ilikuwa mimi na wenyeji wangu watatu. Miundombinu ya Vic Falls imeboreshwa sana na vilevile kuna huduma za vyakula, vinywaji na maduka ya sanaa za mikono. Jambo linalomfanya mtu kustareheka baada ya kuyaona maporomoko.
Nikiwa na timu ya Urithi Tours baada ya kuona maporomoko ya Kalambo.
Nimeandika simulizi hii ndefu, kama sehemu yangu ya wajibu kama Mtanzania kuitangaza vema nchi yangu. Vilevile, kama rai kwa mamlaka zinazohusika, makampuni ya huduma za utalii na wananchi wenzangu, kuhakikisha tunatangaza vema juu ya vivutio vya kipekee tulivyo navyo. Jambo ambalo sikuwaza, ni kuwa mkoa wa Rukwa una vivutio vya kipekee mno.
Nitakuandikieni simulizi nyingine juu ya safari yangu ziwani Tanganyika.
Wakati Tanzania ikijiandaa kushuhudia fainali za Azam Sports Federation Cup zitakazofanyika uwanja wa Nelson Mandela mjini Sumbawanga mwezi Mei mwaka huu, ninapendekeza kwa kila mwenye kuja Sumbawanga kuona fainali hizi, walau atenge muda wa kutembelea vivutio hivi vya utalii. Ambavyo, ni vya kipekee kabisa.
Nikutakieni mchana mwema.
Fadhy Mtanga,
Sumbawanga, Rukwa.
Jumatatu, Februari 17, 2020.
Tazama zaidi video ya Kalambo hapa chini