Mnamno tarehe 19 June 2019 mida ya Saa tisa alasiri tukiwa ofisini kwetu Studio Native Maeneo ya Block T Mbeya Mjini tukiendelea na Shughuli zetu za kila siku za Upigaji Picha mimi na wafanyakazi wenzangu watatu ambao ni Shah Mjanja, Bright Nyondo Na Yohana/Mufasa. Tulipata wazo la kwenda Mlima Loleza Mlima huu unapatikana Jijini Mbeya wenye urefu wa mita 2656 juu ya usawa wa Bahari. Mlima huu ni mlima wa tatu kwa urefu mkoani Mbeya.

Mlima huu una njia kuu tatu zilizo maarufu zaidi.

01: Njia ya kwanza ni njia ya wapita kwa miguu njia hii safari yake unaanzia Rufaa hospitali mpaka kileleni utatumia Masaa matatu (3) Na dakika Hamsini na Moja (51) Ina umbali wa (Km 14).

02: Njia hii ya pili ni Barabara ya umbali wa dakika 46 (Km 18) kutokea Rufaa Hospitali lakini njia hii ni kwaajili ya magari makubwa yaani (4×4) sio rafiki kwa magari madogo. Pia kwa miguu utatumia masaa mawili na dakika 57.

03: Njia ya tatu Nusu ni Barabara ya kiwango cha Lami na nusu nyingine ni kiwango cha changalawe njia hii kwa Gari ni Km 15 umbali wa dakika 38 kutokea Lift Valley Hotel mpaka kilipo kilele cha mlima Loleza kupitia Kawetire.

Bhasi sisi tukachagua kupita njia ya Rufaa Hospital kutest gari la ofisi aina ya Land Rover 110 Tdi. Wazo hili lilikuja Baada ya Bwana Shah Mjanja kutupa habari kuwa Mafundi wamempa taarifa kua tayari Gari imetengamaa

tokea imefanyiwa matengenezo ya gear box iliyokua ikisumbua hapo mwanzo. Unajua kwanini tulichagua kwenda Loleza kupitia barabara ya rufaa hospitali? Jibu ni kuwa tulichagua barabara hiyo sababu ni barabara korofi sana inahitaji gari iliyo juu pia iwe na nguvu sana ya kuimili miinuko mikali na mashimo. Tulikua na uwezo wa kupiła barabara ya kawetire ambayo takribani Nusu ya safari ni barabara ya kiwango cha lami na kipande kingine ni barabara ya kiwango cha Changalawe lakini tulikua na imani tusinge furahia wala kuona uwezo wa Land Rover Defender Kama tujuavyo Land Rover ndio mbabe wa gari nyingi za barabara korofi za Africa. Basi mida ya Saa tisa na nusu alasiri tulianza safari yetu taratibu kuelekea mlima loleza kupitia njia ya rufaa ni safari ya takribani Dakika Arobaini na Sita (46) kufika kilele cha mlima Loleza tukiwa njiani tukikalibia kileleni tuliweza kuona Muonekano mzuri sana wa mlima wa pili kwa urefu mkoani Mbeya mlima huo unaitwa Mlima Mbeya Wenye Urefu wa Mita 2,320 Juu ya Usawa wa Bahari.

Tukasimama kupiga picha hiyo hapo chini.

Picha hii huyo hapo Pichani ni Yohana/ Mufasa akiwa mbele ya Land Rover akitazama jua likizamia Juu ya kilele cha Mlima Mbeya Picha hii niliipiga majira ya saa 11:23:55 Jioni. Tarehe 19/06/2019.

Baada ya kupiga hii picha tuliendelea na safari kuelekea kilele cha Mlima Loleza tuliweza kufika kileleni Saa 11:57:50 Niliona muonekano malizawa wa kilele cha Mlima Mbeya Kutokea Loleza Moja kwa moja nilishuka Kwenye Gari na kuanza kupiga picha maana sikutaka kupoteza muda kwasababu uzuri wa eneo hili ulikua sio kifani na jua lilikua linakwenda kuzama liliongeza nakshi zaidi ya muonekano wa mlima Mbeya kutokea Mlima Loleza. Unaweza ukatizama uzuri huu ambao nakusimulia kupitia hizi Picha hapa chini.

Picha hii ni Muonekano wa Mlima Mbeya kutokea kilele cha mlima Loleza. Hii picha nilipiga majira ya Saa 12:00:00 Jioni, tarehe 19/6/2019.

Picha hii ni Muonekano wa Mlima Mbeya kutokea kilele cha mlima Loleza. Hii picha nilipiga majira ya Saa 12:00:06 Jioni.
Tarehe 19/6/2019.

Baada ya mimi kupiga hızo picha kadhaa kila mmoja wetu alikua na wazo lake kichwani nini kifanyike tukiwa hapo kwenye kilele cha mlima Loleza Wazo la kwanza lilitoka kwa
Shah: Buddah mahala hapa panafaa sana kwa kufanya camping

Mufasa: Ndio Kigogo panafaa sana ila kwa hii baridi tunaweza tukaganda hapa Wote: Tukaangua kicheko

page3image32884816

 

Bright: Lakini ukiwa ndani ya Tent umejifunika vizuri hutohisi baridi. Mimi: Mmmmh labda uwe na Miwa (Kvant) au Whiskey Kichwani maana hii baridi kama tupo Nchi za Scotland huko
Mufasa: Ahahahahhaha Buddah umeongea ukweli.
Shah: Embu bwana Bright tujaribu kufunga Tent tuone.
Mimi: Hapo kwa majaribio sawa.
Bhasi kwenye Gari kulikua na baadhi ya Tents kadhaa kama ilivokawaida tukashusha Tent moja na kuanza kuzifunga kwaajili ya majaribio kama unavyoona hapo chini kwenye picha.

Picha ili niliipiga majira ya Saa 12:07:49 Jioni.
Tarehe 19/06/2019.
Gari aina ya Land Rover pembeni Bwana Bright na Mufasa wakiendelea na shughuli za kufunga Tent.

Picha: Gari aina ya Land Rover pembeni Bwana Bright akiwa mbele ya Gari akijaribu kupiga picha na Simu yake. Mufasa na Shah wakipiga soga mbili tatu kuhusu mlima Loleza.

Picha: Mufasa na Bright wakiwa mbele ya Gari wakitaka kurusha Drone ili kupiga picha ya Mlima Loleza pembeni Shah akijaribu kuuliza maswali mawili matatu kuhusu maeneo haya kwa Mlinzi wa minala ya simu iliyopo kwenye kilele hichi cha mlima Loleza. Nyuma zaidi unaonekana Mlima Mbeya.

Picha: Bright akiwa ndani ya Tent pembeni Mufasa,Mlinzi na Shah wakijadiliana baadhi ya Mambo kuhusu kurudi eneo hili mara ya pili.

Ukiwa Juu ya kilele cha Mlima Loleza Utaweza kujionea karibia Mji mzima wa Mbeya kuanzia Uyole mpaka Songwe. Na majira mazuri ya kwenda hapo mlimani ni mwezi wa sita (6) mpaka wa kumi na moja (11).
Baada ya shughuli za Picha kumalizika tuliweza kuondoka hapo kileleni majira ya Saa Mbili usiku kulejea Mjini kupitia njia ya kawetire. Tukiwa njiani Maongezi yetu makubwa ilikua kulejea Mlima Loleza siku zijazo tukiwa tumejipanga vizuri na Blanketi kwaajili ya kujikinga na baridi pia Vyakula na Vinywaji pindi tutakapo fanya Camping Pamoja na marafiki kadhaa ambao tutawaalika nao wajionee uzuri wa mlima Loleza.

Makala haya yameandikwa na Issa Millanzi

Issa ni mpiga picha mashuhuri jijini Mbeya na Dar es Salaam, kwa shughuli za harusi na matukio ya kitaalamu pamoja na safari.

Instagram: (@thatmbeyaguy @issamillanzi)
Simu:  +255683103780
Email: issa@everydaymbeya.com