IMEZOELEKA kwa watu wengi kutembelea maeneo kadha wa kadha ndani na nje ya Tanzania ifikapo mwisho wa mwaka. Mwezi Disemba ni mwezi wa likizo na sikukuu. Ukiondoa shule ambazo ni kawaida kwenda likizo ya mwisho wa mwaka, taasisi nyingi hufunga ofisi zao juma la mwisho la Disemba kwa ajili ya sikukuu za Noeli na Mwaka Mpya. Ndiyo maana, si jambo la ajabu kwa mwezi Disemba kufahamika kama mwezi wa sikukuu.

Mwaka 2020 umekuwa na makandokando mengi. Wakati mwaka ukiwa ndiyo kwanza unakolea mwendowe, dunia ikapatwa mazongezonge ya UVIKO (COVID-19). Shughuli zikasimama karibia dunia nzima. Taasisi zikatetereka kiuchumi. Na vivyo hivyo, watu binafsi. Wapo waliopoteza kazi kwa sababu iliwalazimu waajiri wao kupunguza gharama za uendeshaji. Wapo waliofunga biashara zao kwa sababu ya kukosekana kwa wateja ama bidhaa. Wapo waliowapoteza ndugu zake. Mambo hayakuwa mambo.

Pamoja na hayo yote, mwaka sasa unaelekea ukingoni. Juma lijalo, tutaingia mwezi wa Disemba. Ni wazi, utatamani kwenda mahali ukafurahie mwisho wa mwaka na ndugu, jamaa na marafiki. Lakini, maroroso ya mwaka huu yamekupunyua hasa mifuko yako, na ungetamani kwenda mahali pa karibu, ama pa gharama nafuu upate kufurahia na wale uwapendao.

Nami leo, nimekuandalia maeneo 10 yaliyopo Nyanda za Juu Kusini, unayoweza kutembelea pasipo kulazimika kutumia gharama kubwa. Nikitumia uzoefu wangu wa kusafiri, ninakuhakikishia haya ni maeneo ambayo hutojutia kwenda. Yatakupa wewe pamoja na wale uwapendao starehe kubwa ya akili yako. Ili sasa, unaporejea ofisini mwaka mpya wa 2021, akili yako iwe safi tayari kwa kuanza kupokea yale ambayo mwaka ujao utatuletea. Ninafahamu kuna maeneo mengi ambayo umekwenda ama umeyasikia. Ukiachilia mbali hayo, yapo haya 10 niliyokuchagulia leo.

1.Ufukwe wa Matema

Ufukwe huu wa Ziwa Nyasa ni maarufu sana. Upo mkoani Mbeya. Unafikika kwa urahisi sana kutoka Mbeya mjini. Umbali wake ni takribani kilometa 150 kutoka Mafiat, Mbeya huku barabara yote ikiwa na lami safi kabisa. Manufaa ya kuchagua kwenda Matema Beach hayaishii ufukweni kwenyewe. Barabara kuu ya Tanzania-Malawi imepambwa kwa sura ya nchi na uoto wa asili na wa kupandwa wenye kuvutia sana mboni za macho yako. Utapata fursa ya kupandisha na kushusha milima iliyopambwa kwa miti, migomba, viazi, chai, michikichi, mpunga na kokoa.


Hebu ona mwenyewe!

Si hivyo tu, taswira ya safu za Milima ya Livingstone zitayastarehesha macho yako sehemu kubwa ya safari yako. Inavutia ee!

Ukiwa ufukweni Matema, utaburudishwa na mandhari ya kipekee ya ziwa chini ya safu kubwa za milima hiyo ya Livingstone. Maji ya Ziwa Nyasa ni masafi sana wakati mwingi, isipokuwa tu kama mvua itanyesha sana ama ziwa kuchafuka kwa sababu kadha wa kadha za kijografia. Ukiwa Matema Beach, utapata uchaguzi wa huduma za hoteli kadhaa zilizipo. Kuna michezo chungu-mbovu ya kukufanya wewe na wenzako muwe na wakati muruwa kabisa.


Ziwa Nyasa

Usiishie tu ufukweni, nenda safari ya boti ama mtumbwi hadi ufukwe wa upande mwingine ukawaone samaki wa mapambo. Siyo tu kuwaona samaki hao waliopambwa kwa rangi zenye kuvutia kama nyekundu, njano, bluu, urujuani na zinginezo, vilevile utayaona mawe ya mapambo yakiwa lukuki. Sitoshangaa ukiyabeba machache ukayapambe nyumbani kwako.


Wallpaper ya simu yako. Hapo je! Jamani

Zaidi ya yote, safari ya Matema itakupa fursa ya kula wali mtamu sana kwa samaki kutoka ziwani humo. Umewahi kumsikia samaki Mbasa? Maneno hayatotosha kuuelezea utamu wake. Lakini pia, kuna dagaa watamu sana. Wanaonoka kutafunika wakiwa wakavu pasi kupikwa, ama, wakikaangwa.

Bila shaka ukiwa shule umewahi kusoma kwenye somo la Historia habari za Wakisi na biashara zao za vyungu kutoka milimani hadi Kyela. Sasa basi, ukienda Matema Beach likizo hii, utapata fursa ya kununua vyungu mbalimbali vya mapambo na kupikia. Utajisikiaje nyumbani kwako ukiwa na maua na mimea kama cactus? Vyungu vya Wakisi vinakupa fursa adhimu ya kupamba nyumbani kwako.


Taswira ya kupendeza machine pako

Uzuri wa safari ya Matema Beach, unao uchaguzi wewe mwenyewe kama ulale hukohuko ama ushinde tu kutwa nzima na kurejea siku hiyohiyo kadri ya bajeti yako. Na endapo mtaamua kulala, ukiachilia mbali hoteli zilizopo, mnaweza kwenda na mahema ili kupunguza gharama.

2.Viewpoint

Je, unafahamu kuwa barabara iliyo juu zaidi Tanzania ipo mkoani Mbeya? Bila shaka wakati ukisoma Jografia shule ya msingi na sekondari ulipata kusikia juu ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki. Sikuulizi ili ufanye mtihani wa NECTA ama UE; la hasha! Usingetamani likizo hii uone mandhari ya kuvutia ya bonde hili lililoanzia huko Bahari ya Shamu na kupita maeneo kadhaa ya Tanzania kabla ya kwenda kupotelea huko Msumbiji na kuingia Bahari ya Hindi. Usiogope, sikusudii kukurudisha darasani.

Viewpoint ni eneo lililopo takribani kilometa 25 kutoka Mbeya mjini ukishika barabara iendayo Chunya, kitovu cha dhahabu. Kwa hizo kilometa zote, utapandisha safu za milima ya Mbeya hadi uende juu kabisa ambako ndicho kilele cha barabara za Tanzania. Nina hakika utatamani kupiga picha kwenye kibao chake.

Kisha, safari inongeshwe na mandhari si tu ya miti, bali pia, mwonekano wa kusisimua wa bonde hilo maarufu duniani. Hii si safari ya gharama. Lakini, nakuhakikisha kiwango cha burudani utakachokipata, hutoweza kukielezea kwa maneno.

Ufanye nini ukifika Viewpoint? Piga picha za kutosha kwenye ukingo wa bonde hilo, kitaalamu Chunya Escarpment. Kuna baridi ya kusisimua eneo hilo. Usiogope. Inaburudisha na kuchangamsha akili.


Sema Mwenyewe!


Kona za kupendeza

Ukiwa hapo na wenzako, mnaweza kula chakula mlichokifunga kutoka mjini. Lakini je, wewe na jamaazako msingetamani kwenda na jiko lenu mkachomea nyama pale? Msisahau kubeba na vinywaji vya kuwatosha. Na simu zenu, ziwe na GB za kutosha za kutunza picha za kumbukumbu

.
Kona kama zote

Muda ukiwaruhusu na mafuta ya gari yakiwatosha, kwa nini sasa msifike Chunya mjini? Msingependa kuuona mji huo uliouzaa mji wa Mbeya? Mji wa dhahabu. Nyamachoma ya Chunya ni tamu asikwambie mtu. Niamini mimi!

3.Ruaha River Valley

Kama hufahamu, naomba nikufahamishe leo. Kwamba, takribani kilometa 10 kutoka Iringa mjini, ama mbele kidogo ya Kituo Kikuu cha Mabasi Igumbilo, ukiwa unakwenda Dar upande wa kulia, kuna bonde zuri mno la Mto Ruaha. Ni eneo la kupendeza sana. Bustani nzuri ya nyasi na mpangilio wa majengo yake, vitakupa furaha na sababu ya kutembelea.


Panapendeza

Kama unapenda samaki, basi nakuhakikisha samaki wa River Valley utashindwa kummaliza kwa sababu ya ukubwa wake. Ama, kitu pekee kitakachokufanya ujilazimishe kummaliza ni utamu wake. Eneo hili ni zuri sana kwenda na familia yako, ndugu, jamaa ama marafiki. Unaweza kuchagua kwenda asubuhi na kurejea jioni.

Lakini, kwa nini tu usiamue kwenda kulala? Hutotamani kuona mandhari ya kuvutia ya jua linapozama?

Ukiachia mbali starehe ya mahali hapo inayojumuisha michezo kama bembea, ni vema kwenda kuyaona maporomoko ya Mto Ruaha. Mto huu ni miongoni mwa mito mikubwa sana Tanzania, ukiyapeleka maji yake kwenye Mto Rufiji ambao nao huyapeleka Bahari ya Hindi.

Wakati mkienda zenu kuona maporomoko, mtapita kwenye mashamba ya kahawa yenye mandhari ya kuvutia. Kama mnapenda mvinyo, basi msiache kutembea nao. Kule kwenye maporomoko, kuna meza nzuri ya mbao juu ya mawe juu ya mto. Italeta burudani nyingine ya kusisimua.


Usingependa kuala na mwenzako hapo?


Na chupa ya mvinyo

4.Mufindi

Bila shaka umewahi kusafiri barababara kuu ya Tanzam. Ama kwa kifupi, barabara ya kutoka Iringa mjini hadi Makambako na Mbeya. Bila shaka tena, umeiona misitu ya Sao Hill. Kuna ile mandhari ya lile bonde lenye maji. Huwa haikuburudishi taswira yake?

Sasa nikwambie. Ukiingia ndani kutoka pale Mafinga mjini ama Nyololo/Igowole utakutana na mashamba makubwa ya chai na misitu. Umewahi kupigia picha kwenye mashamba ya chai yanayopendezesha safu za milima? Bila shaka bado.

Basi, moja ya maeneo ninayoyapendekeza kwako kuyazuru Disemba hii, ni Mufindi.


Inapendeza

Kuna raha ya aina yake kama utafanya safari kwenye barabara ya vumbi (sasa haina vumbi kwa kuwa mvua zimeanza) katikati ya misitu ya miwati na milingoti na mashamba ya chai. Halafu, safari yenu ikaishia Mufindi Highland Lodge ama Mufindi Farm Lodge.

Unadhani tu itakuwa imetosha?

La hasha!

Mkiamua kwenda safari hii, mtapata burudani ya kuendesha farasi, kuvua samaki, kucheza tenisi, kuendesha baiskeli na vilevile kutembelea mambo ya kitamaduni kwenye jamii eneo hilo. Kama hufahamu, wilaya ya Mufindi inayakutanisha makabila makubwa matatu; Wabena, Wakinga na Wahehe.

5.Ziwa Tanganyika

Ni ajabu hata kuliweka namba 5 kwenye orodha yangu! Ni kwa vile tu, orodha hii haijaandikwa kwa kipaumbele. Kama ningetaka kuandika kwa kufuata kipaumbele, Ziwa Tanganyika ni kipaumbele changu namba moja. Hebu mwenyewe fikiria, hili ni ziwa la pili kwa ukongwe ulimwenguni. Ni ziwa la pili kwa ukubwa duniani. Na kama haitoshi, ndilo ziwa la pili kwa kuwa na kina kirefu zaidi ulimwenguni. Halafu, lipo Tanzania!

Huko juu nimezungumza habari za Bonde la Ufa la Afrika Mashariki. Ziwa hili, ni miongoni mwa maziwa yaliyomo kwenye bonde hili. Ni ziwa kubwa hasa. Limezungukwa na nchi nne. Kule Kaskazini kuna Burundi; Magharibi yake kuna Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo; Kusini ipo Zambia; na, Mashariki mwa ziwa hili ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuna simulizi nzuri kuhusu ziwa hili. Mji wa Kigoma, samaki Migebuka, Hifadhi ya Taifa ya Mahale, Kisiwa cha Lupita na kadhalika.

Mimi leo, nataka kukwambia maeneo mapya unayoweza kuyatembelea.

Eneo la kwanza ni kijiji cha wavuvi cha Samanzi. Karibia kilometa 40 baada ya kuchepuka barabara kuu ya kwenda Bandari ya Kasanga. Safari hii itaanzia Sumbawanga mjini. Ni miongoni mwa miji mizuri sana ya Tanzania. Ni safari ya aina yake. Ukifika kijijini Samanzi, omba wenyeji wakupeleke kwa boti kuyaona mapango ya Ziwa Tanganyika.

Ni safari yenye kuvutia sana. Kwa kuwa boti zao ni kubwa, mtaongozana na wanakijiji wengine huku mkipeana michapo ya kila rangi.

Mkimaliza kuona mapango, mkiwa njiani kurejea Samanzi kijijini, mtasimama kwenye ufukwe wa mawe ya mapambo.


Mawe ya Mapambo


Unataka kubeba?

Je, hamtopenda kuyapiga picha kwa ajili ya wallpaper kwenye simu zenu na tarapakato? Hiyo haitotosha. Ninaamini mtabeba mawe kidogo mkayapambe majumbani ama ofisini kwenu.

Agizeni kabisa kwa mwenyeji wenu muandaliwe ugali kwa samaki. Nakuhakikishia, mtakula kila aina ya samaki anayevuliwa ziwani humo.

6.Korongwe Beach

Ingawa hili eneo lipo kwenye ufukwe wa Ziwa Tanganyika, ninalipa umuhimu wa kipekee sana. Ni eneo bikra kwenye tasnia ya utalii. Hakuna shughuli zozote za utalii zinazofanyika kwenye ufukwe huu wa aina yake. Mandhari ya ufukwe inavutia sana.


Ufukwe wa kuvutia

Ufukwe una mchanga mzuri kwa rangi na hisia zake. Lakini kama haitoshi, kuna mawe yaliyopangika vema ndani na nje ya ziwa. Kuna jiwe moja kubwa ambalo wenyeji hupanda juu na kucheza bao ama lova.


Jiwe kubwa la kupungia upepo wa ziwa

Msingetamani kuweka hema na kulala juu ya mwamba huo unaopewa kivuli na mti mkubwa juu ya mwamba? Pembezoni kuna boti na mitumbwi ya wavuvi. Kuna eneo zuri la kuogelea pembezoni mwa miamba hiyo.


Raha ya michezo juu ya jiwe

Utalii mwingine wa Korongwe ni utamaduni wa kuandika mawe. Mawe yote hata yale yaliyo mbali ziwani yamepambwa kwa maandishi ya rangi za mafuta yaliyoandikwa kwa ustadi. Ni eneo linalofaa kwa picha kali za kuringishia kizazi hiki na vijavyo.

Mkiwa Korongwe, pembezoni kidogo tu mwa ziwa, mtawaona wenyeji wakiwakausha samaki kama migebuka. Fikiria, hao samaki na kaugali kako fulani hivi! Ooooh! Unangoja nini kwenda?

Uzuri wa safari ya kwenda Korongwe ni kupita Mbuga ya Lwafi. Mbuga hiyo inapakana na Hifadhi ya Taifa ya Katavi. Hivyo, hutoshangaa nikikwambia uwezekano wa kuwaona wanyama kadhaa mkiwa njiani. Jambo nililolipenda zaidi ni mbwembwe za kuruka za ndege tai. Anaruka na kuganda hewani mbele ya gari lenu.

Safari ya kwenda Korongwe ni ndefu kidogo. Takribani kilometa 180 hivi kutoka Sumbawanga mjini. Barabara ni nzuri. Kilometa 150 hivi ni za lami. Zinazobakia ni za vumbi lakini barabara iliyochongwa vema. Safari hii itakupitisha mji wa Namanyere, wilayani Nkasi. Ama, kama mtapita njia ya mkato, mtapita Chala. Usingependa kununua asali bora kabisa?

7.Kalambo Falls

Kila mtu angenishangaa endapo kwenye orodha yangu ya maeneo 10 ya kuyatembelea Nyanda za Juu Kusini nisingeiweka Kalambo Falls. Ni mahali ninapopapenda sana.

Ni umbali wa takribani kilometa 100 kutoka Sumbawanga mjini. Kwa takribani kilometa 83 ni lami tupu. Unachepukia Kisumba. Raha ya safari hii ni kupita kwenye mbuga yenye tembo wakubwa. Mkiwa na bahati siku hiyo, mtakutana na tembo.

Maporomoko ya Kalambo yanatokana na Mto Kalambo. Mtu huu unazigawa Tanzania na Zambia. Ndiyo maporomoko makubwa zaidi barani Afrika yakiwa na tone moja. Unashangaa? Bila shaka umesikia sana kuhusu Victoria Falls ama Mosi-0a-Tunya kwenye mpaka wa Zambia na Zimbabwe. Sahau kuhusu hilo. Urefu wa Kalambo Falls (mita 235) ni zaidi ya mara mbili ya urefu wa Victoria Falls (mita 108). Upana wa Gema la Kalambo ni kilometa 1 huku maji ya mto huo baada ya kuporomoka, yanasafiri umbali wa kilometa 5 kabla ya kutiririka kwenye Ziwa Tanganyika.

Kwa nini uende Kalambo?

Kila kitu kinasisimua. Utashuka ngazi 118 ili kuuona ukingo wa Gema la Kalambo ambako ndiko maji yanaanza kuporomoka. Kwa mbali, unaliona Ziwa Tanganyika. Kisha badala ya kupandisha ngazi kurudi mlikotoka, mnapandisha mlima kidogo pembezoni mwa gema hilo huku mkiendelea kustareheshwa na taswira ya mvuke wa maporomoko.


Ule moshi ule!

Mkifika kwenye kituo kikuu cha Kalambo Falls juu kabisa, ndipo safari ya kushuka ngazi 870 inaanza. Sijakosea, ni mia nane na sabini. Wala usiogope. Ni uzoefu wa aina yake. Kama una wasiwasi kuchoka, si vibaya kutembea na glukosi ama chupa ya maji.


Ngazi 870

Chini kabisa, mtaiona taswira ya aina yake ya maporokomo. Ushawahi kuziona nyasi zinazotembea? Bila shaka, hapana. Basi nakwambia, ukiwa pale chini, lazima macho yako yazione nyasi zinazotembea. Zinatembeaje? Usiache kufika Kalambo Falls.


Ewaaa!


Hapo Vip!

Bila shaka, baada ya safari hii mtapenda kulala Sumbawanga mjini. Ni mji mzuri sana kama nilivyoandika mwanzo. Kuna mahali pa kula pazuri pengi. Kila aina ya vyakula kuanzia vya Kiswahili hadi Bara Hindi.

Bei ya chokoleti na almond mjini Sumbawanga ni ya chini kuliko miji mingine nimetembelea Tanzania. Hutopenda kununua zawadi kidogo kwa wapendwa wako?

8.Ziwa Kisiba

Nina hakika umewahi kusikia kitu kinachoitwa ‘volkano’. Kwa mfano, kwamba Mlima Kilimanjaro (mlima mrefu zaidi Afrika) ni wa volkano. Umewahi kusikia juu ya ziwa la volkano? Nisisitize, sikusudii kukurudisha darasani kusoma Jografia. Nakusudia kukupa burudani ya kumalizia mwaka.

Mkoani Mbeya, na hususani wilayani Rungwe lipo Ziwa Kisiba.


Ziwa Kisiba

Ni ziwa lenye simulizi nyingi sana. Kwa mfano, kuna simulizi kuwa wakoloni Wajerumani waliacha mali nyingi ziwani humo. Simulizi hizi hazijathibitishwa kisayansi. Lakini, ni ziwa lenye mto wa chini kwa chini. Ziwa hilo limezungukwa na milima yenye uoto wa asili pande zote.

Watu wengi huzungumzia habari za Msitu wa Magoroto, mkoani Tanga. Wacha nikwambie, utalii kwenye ziwa hili unakuwa kwa kasi sana. Tayari miundombinu imeboreshwa ili kukupa uzoefu wa kutosha kusimulia vizazi vyako. Safari ya Ziwa Kisiba si lazima mkalale. Mnaweza amua kwenda asubuhi na kuondoka jioni.

Lakini nikuulize, wewe na wenzako msingependa kufaidia jua linapozama? Taswira ya machweo kwenye ziwa hilo ni ya kipekee sana. Kwa wale wenye kupenda picha za mawio na machweo kama mimi, hapa si pa kukosa.

Upande wa pili kuna uwanja wa mpira. Ingependeza mkafanya michezo ya kuwatosha. Bado sijazungumzia kupiga makasia ziwani na kulala kwenye mahema.

9.Daraja la Mungu

Mungu alijenga lini daraja? Unaweza kuniuliza hili swali. Ama, Mungu alilijengaje?

Mto Kiwira, unaotiririsha maji yake kutoka kwenye matawi yanayoanzia kwenye Mlima Rungwe na safu za Milima ya Uporoto, unayo maajabu mengi sana. Miongoni mwa maajabu hayo, ni Daraja la Mungu lililopo karibu na Chuo cha Magereza Kiwira. Daraja lipoje? Ni mwamba mkubwa ulipasuliwa na nguvu ya mto huo. Wilaya ya Rungwe imetawaliwa na sifa za volkano. Basi ule uji wa volkano (lava) ulipigwa dafrao na maji hayo kiasi cha kuunda daraja la asili kubwa ambalo binadamu na wanyama wanapita juu yake pasipo shida yoyote.

Ni eneo zuri sana kupigia picha na kuburudika. Ukiachia mbali daraja hilo la asili, pembeni kidogo kuna daraja la binadamu linalokuwezesha kuona taswira nyingine ya daraja hilo la Mungu.

Safari ya Daraja la Mungu haitopendeza kuishia hapo. Mbele kidogo kuna Kijungu. Hiki ni chungu cha asili ambako maji yote ya mto Kiwira yanaingia humo na kupotea chini ya miamba kabla ya kuibukia mbele kidogo na kuendelea na safari yake kuelekea Ziwa Nyasa.

10.Kaporogwe Falls

Hii ni orodha ya tano kutoka mkoani Mbeya. Inatokana na upekee wa Mbeya kuhusiana na maeneo yanayovutia.

Takribani kilometa 25 kutoka Tukuyu mjini, Kaporogwe ni tawi la mto Kiwira (ule mtu niliokwambia unayo maajabu mengi yenye kuvutia). Ni eneo lenye taswira ya kuvutia mno. Mwamba mkubwa umejigawa katikati na kutengeneza mfano wa jukwaa. Hebu fikiria, wewe na wenzako mketi kwenye hilo jukwaa mkiburudikwa kwa vyakula, vinywaji na muziki huku mkiyatazama maji yanayoporomoka mbele yenu. Si taswira ya kuvutia?

Maji ya mto Kakala yanapodondoka

Halafu, baadaye mshuke chini maji yanakoporomokea zaidi muufaidia mvuke wake wenye kusisimua vilivyo. Aaah, raha iliyoje!

Safari ya Kaporogwe Falls itakupeni fursa ya kuziona kwa uzuri safu za Milima ya Livingstone zilizopambwa kwa uoto wa asili wenye maua na miti; sambamba na mazao kama chai.

Kazi ni kwako, na, kupanga ni kuchagua!

Nimalizie kwa kusema, maeneo haya 10 yaliyopo Nyanda za Juu Kusini si hayo tu unayoweza kuyatembelea likizo hii. Yapo mengi kama Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Kisolanza Farm, Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, Utengule Coffee Lodge, Hifadhi ya Taifa ya Katavi, Ngonga Beach, Ziwa Ngosi, mji wa Tunduma na Nakonde na mengineyo mengi.

Ukihitaji maelezo zaidi juu ya maeneo haya waweza kuwasiliana nami kwa simu na barua-pepe, ama na makampuni kadha wa kadha ya utalii kwenye miji ya Iringa, Mbeya na Sumbawanga. Makala yangu imelenga kukupa ufahamu wa jumla na kukushawishi kutembelea maeneo haya.

Nikutakie mipango mizuri na maandalizi mema ya safari za mwisho wa mwaka. Panapo majaaliwa, nitakuandia juu ya maeneo mengine ya kuyatembelea.

Ndimi msafiri mwenzako,

Fadhy Mtanga,

Mbeya, Tanzania,

Alhamisi, Novemba 26, 2020.

© Haki zote zimehifadhiwa. Picha zote zilizotumika kwenye makala hii, isipokuwa ilipoelezwa tofauti ni mali ya Fadhy Mtanga. Si ruhusa kuzitumia mahali pengine pasipo idhini ya maandishi.