Bhujonde ni fukwe katika Kijiji cha wavuvi na sehemu nzuri ya kutazama mto Kiwira unapoingia ziwa Nyasa.

 

Ukiwa Mbeya, ardhi yake imejazwa na maji mengi, katika maporomoko, mito, maziwa na hata huko mapangoni; na hizi ni moja ya sababu tele za kutembelea mji huu mzuri kusini kabisa mwa Tanzania. Lakini utahitaji kufahamu wapi pa-kwenda. Makala hii inaangazia maeneo ambayo utapata wasaa murua wa kufurahia ‘nature’ na maji yake katika ubora.

Sehemu hizi zinaweza kufikiwa wakati wote wa mwaka lakini zinapendeza sana wakati wa masika, wingi wa maji huyajaza maporomoko na mito, hufanya maji yawe maji haswaa. Kwahiyo, wakati mzuri sana ni kati ya mwishoni mwa Novemba hadi mwanzoni mwa mwezi wa Aprili, lakini wakati mwingine unaosali pia unafaa kutembelea sehemu hizi.

  1. Maporomoko ya Kaporogwe

Maporomoko haya yapo kijiji cha Isibu takribani kilomita 18 kutoka mji mdogo wa Ushirika wilayani Rungwe, Yanatokana na anguko la mto Kala unaoanzia milimani wilayani Rungwe, lakini maporomoko ya Kaporogwe hayaonekani kuwa maporomoko yanayotembelewa sana katika mkoa wa Mbeya licha ya maumbile yake yenye kushangaza. Zipo hadithi za masimulizi mengi lakini sifa yake kuu ni nafasi wanayopata wageni ya kuyatazama kutokea ndani na nje.


Muonekano wa maporomoko kutokea ndani ya  pango.


Muonekano wa maporomoko kutokea nje ya pango.

Licha ya kuwa kivutio hiki kinasimamiwa na halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, lakini mara nyingi tulizofika hatukumkuta msimamizi rasmi wa halmashauri. Ukifika Kaporogwe utakutana na wanakijiji wakiwemo rafiki zetu Ras Mwakalinga, Geofrey, Bonifasi na wengineo. Hivyo, usiogope, watakudumia kwa kukupa maelezo muhimu na hadithi zinazovutia kuhusu Kaporogwe.

Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe hutoza tozo kwa wageni wanaotembelea maporomoko ya Kaporogwe.

2. Ziwa Kisiba


Huyu Kisiba anashikilia rekodi lukuki, lakini chache ni upana wake wa mita 600 na kina kirefu cha mita 70. Ni ziwa la volkano lilioundwa miaka tele iliyokwenda. Lina maji tulivu sana yenye mawimbi yasiyoweza kuonekana, linao uhai wa samaki wanaoweza kuonekana kwa urahisi na hadithi za mali tele zisizoonekana toka kwa mkoloni zinaz0semekana kuhifadhiwa ndani yake miaka ya kale.

Ziwa hili ni zuri na salama kwa kuogelea kutokana na maji yake masafi yasiyo na dhoruba.


Ziwa Kisiba linafaa sana kwa matembezi ukiwa na rafiki zako, kwa ajili ya matembezi ya kawaida au tafrija. Fikiria kwenda ziwani na marafiki zako katika mapumziko ya mwishoni mwa wiki!

Ziwa Kisiba lipo kilomita 80 kutoka Mbeya mjini kupitia barabara iendayo Malawi katika wilaya ya Rungwe huko Tukuyu.

3. Maporomoko ya Mwakipembo, Kitulo.

Maporomoko haya yapo katika hifadhi ya Taifa ya Kitulo inayojulikana pia kama Serengeti ya Maua, yanapatika kilomita 90 kutoka Mbeya mjini ndani ya hifadhi iliyosheheni uzuri mwingi wa maua zikiwemo aina zaidi ya 45 za Chikanda (Orchids) pekee. Maji ya mto Nhumbe yanafanya maporomoko haya yawe mazuri sana. Ubora wake unaongezewa na uwepo wa kichanja kinachofaa kwa pikniki au stori huku ukifurahia uzuri wa maji na poromoko lake.

3. Matema Beach, Ziwa Nyasa


Matema na fukwe yake ya ziwa Nyasa ni uwanja wa Taifa jijini Mbeya, iwapo umefika Mbeya na hujagusa maji ya ziwa hili wenyeji husema bado hujaifahamu Mbeya. Fukwe hizi ni nyumbani kwa wengi wanaofika kwa ajili ya kupunga upepo wa ziwa, kufurahia mandhari za milima ya Livingstone na kuchezea maji yake, ndani na nje. Hapa ni mahala ambapo wenyeji hufika kila asubuhi kujiliwaza kwa kuogelea, ama kusafiri hadi vijiji vya jirani.

Ziwa Nyasa linao upana wa kilomita 75 na kina chenye urefu wa hadi mita 700 katika baadhi ya sehemu. Ziwa Nyasa ni mojawapo ya maziwa ya bonde la ufa.

Matema ni uwanja wa Taifa unaokutanisha wageni na wenyeji, linazo tunu tele za samaki zikiwemo aina zaidi ya 1000 za samaki aitwaye Mbassa pekee.

Matema kama fukwe ni sehemu bora iliyosheheni huduma zote kwa wasafiri, kuanzia migahawa, hoteli hadi maduka. Ni mahala penye kila kitu kwa ajili ya kila mtu, na ziwa lenyewe linabakia kuwa muhimu kwa kilimo, usafirishaji, uvuvi na starehe zake.


Mbali kidogo na fukwe za Matema kipo kijiji mashuhuri kinachojulikana kwa jina la Ikombe, unaweza kufika Ikombe kwa boti zinazopatikana fukweni Matema. Ukiwa njiani kwenda Matema unaweza kuona samaki wa rangi katika maji ya ziwa.

Jioni ikifika wewe na wenzako mnaweza kutulia fukweni mkajichomea nyama choma pembezoni mwa moto ulioawashwa usiku, huku mwanga wa taa zinazotoka katika boti za uvuvi zikiwaongezea ubora wa mandhari yenu.

Ukiwa Matema au Bhojonde huko ziwani Nyasa hupaswi kulala sana kwa sababu ya ubora wa maumbile yake ikiwemo Mawio na Machweo ya jua, kila siku asubuhi na jioni.

Mawio ziwani Nyasa kutokea fukwe ya Ngonga, ziwa Nyasa

Fikiria mandhari hii ukiwa ziwani!!! Je, nini hasa unataka?

Machweo ziwani Nyasa kutokea fukwe za Bhujonde.

Hakika ziwa Nyasa linavutia.

4. Ziwa Ngosi, Uporoto.

Kusini mashariki kutokea Mbeya mjini lipo ziwa Ngosi, jina maarufu la ziwa lililojipamba kwa ramani ya Afrika. Ziwa Ngosi linatokana na neno la Kisafwa ‘Ligosi’ lenye maana ‘Kubwa’, urefu wake ni kilomita 2.5 na upana wake unafika hadi kilomita 1.6.

Ziwa Ngosi linao muonekano unaoshangaza wageni wengi, limezungukwa na hifadhi ya msitu wa Uporoto wenye aina tele za uoto wa asili wakiwemo nyani.

Utajisikiaje kufika ziwani na kujipatia picha juu ya muonekano huu wa Afrika?

Wasalaam,

Makala hii imeandikwa na Shah Mjanja.

Shah Mjanja ni mpiga picha wa muda mrefu, Muandishi na Mtayarishaji wa makala za televisheni na filamu, Mhifadhi, Mwanamuziki na Msafiri. Ni muanzilishi wa Everyday Mbeya na Studio Native.

Shah Mjanja ni Ofisa wa Habari za klabu ya Mbeya City FC.

Mawasiliano:

Simu: +255-682-326410
Barua Pepe: shah@everydaymbeya.com

Kama kawaida yetu, nakuachia wimbo huu wa Tabu Ley aliyeitwa pia Rochereau ambaye ni mbabe na mbobezi wa muziki wa rhumba kutoka hukoCongo. Wimbo huu ukuliwaze baada ya kusoma makala haya.

Je, unafahamu kuwa Tabu Ley aliwahi kuwa Mume wa Mbilia Bel?

Unalo swali au maoni? Niandikie kupitia shah@everydaymbeya.com au nipigie kupitai simu yangu mkononi hapo juu.