Hello Travellers,

Unasafiri kuelekea Mbeya hivi karibuni na ungependa kutembea mahala panapovutia kwa siku moja? Huu ni mfululizo wa sehemu zitakazokufaa kwa siku moja. Yes! Daytrip with Everyday Mbeya to Rungwe. Chapisho hili litakuonesha mambo ambayo unaweza kufanya kwa siku moja, maeneo, umbali, tozo na uzuri wa mandhari. Mpangilio huu utakusaidia kuua ndege watatu kwa jiwe moja kama waswahili wanavyosema.


Wasafiri wetu katika picha ya pamoja wilayani Rungwe.

Chapisho hili linaangazia maeneo manne pekee yanayopatikana Rungwe. Halitoangazia maporomoko ya Kapiki, Malamba na Malasusa, wala hayatogusia mlima Rungwe na crater zake zingine. Dhumuni la hili chapisho ni kukusaidia kutembelea maeneo ambayo yatakufaa na kukushangaza kwa siku moja pekee.


Muonekano wa Jiji la Mbeya kutokea milima ya Uporoto.

Yafuatayo ni maeneo manne utakayoweza kutalii kwa siku moja pekee

1. Kijungu [Pothole]

Hii ndiyo sehemu inayotembelewa sana kuliko sehemu zote jijini Mbeya kutokana na masimulizi yake, ujirani na njia kuu ya Tanzania Malawi pamoja na ubora wa masimulizi, wakaazi wa Mbeya wanasema iwapo umefika Mbeya na hujafika Kijungu basi hujaifahamu Mbeya kwa uzuri. Neno Kijungu ni jina la Kinyakyusa linalotakana na neno Chungu, sehemu ambayo mto wote wa Kiwira unaingia kabla ya kuendelea na mkondo wake wa asili. Mto Kiwira ni moja ya mito muhimu inayopeleka maji yake ziwa Nyasa. Neno kijungu limetokana na umbile lake la chungu kinachopokea maji.

Kijungu kimetokana na milipuko ya volkano siku za kale.

Kivutio cha Kijungu kinapatikana wilayani Rungwe katika kijiji cha Mboyo kata ya Lufingo, umbali wa takribani kilomita 63 kutokea Mbeya Mjini. Kivutio kipo jirani na chuo cha Magereza kupitia kijiji cha KK mbele kidogo ya Mji mdogo wa Kiwira.

Kijungu kinasimamiwa na halmashauri ya wilaya ya Rungwe ambao pia hutoza tozo kwa wageni wanaotembelea, lakini kabla ya usimamizi wa halmashauri eneo hili pamoja na kivutio cha Daraja la Mungu vilikua chini ya Chifu Mwaihesa wa kabila la Kinyakyusa. Kijungu kinafikika kwa urahisi wakati wote wa mwaka kutokana na ubora wa barabara.

Sehemu hii inafaa kwa picnic, matembezi, upandaji miamba na Utalii wenyewe.

2. Daraja la Mungu (God’s bridge)

Mita chache kusini mwa Kijungu yapo maajabu ya kijografia yaliyounda maumbile ya Daraja la Mungu. Daraja hili limeunda kwa mwamba wa mawe wenye urefu wa mita kumi na mbili na upana wa mita tatu. Jina la daraja hili limetokana na maumbile yake na kwa miaka mingi limekua kiunganishi muhimu kati ya vijiji vya Mboyo na Lugombo.

Daraja la Mungu limetokana na milipuko ya volkano siku za kale.

Wageni wetu wakitazama Kijungu na Daraja la Mungu

Watu wa kwanza kutumia daraja hili ni kabila la Wandali ambao wanapatikana upande wa magharibi wa mto Kiwira. Kati ya mwaka 1930 hadi 1950 daraja la Mungu lilikua kiunganishi cha biashara kati yao na Wanyakyusa walio upande wa mashariki wa Daraja la Mungu.


Daraja la Mungu

Kivutio cha Daraja la Mungu kinapatikana umbali wa takribani kilomita 61 kutokea Mbeya Mjini huko wilayani Rungwe katika kijiji cha Mboyo kata ya Lufingo. Kivutio hiki kipo jirani na chuo cha Magereza kupitia kijiji cha KK mbele kidogo ya Mji mdogo wa Kiwira.

Kutoka Daraja la Mungu hadi Kijungu pana umbali wa kilomita mbili, hii inafanya mgeni anayetembelea Daraja la Mungu aweze kutembelea Kijungu kwa urahisi.


Daraja la Mungu

3. Kaporogwe Falls

Maporomoko ya Kaporogwe ni fahari ya Rungwe. Tofauti na maporomoko mengi duniani, haya unaweza kuyatazama ukiwa nje na kutokea ndani vile vile.

Rungwe ni kisiwa cha mapumziko kusini mwa Tanzania, ni nyumbani kwa Kaporogwe Falls, mojawapo ya kivutio muhimu sana Mbeya na nchini Tanzania kwa ujumla. Kivutio hiki kinapatikana kilomita 18 tu kutokea mji wa Ushirika ulio barabara kuu ya Tanzania Malawi.

Maporomoko haya yanapambwa na uwepo wa pango kubwa linalokupa nafasi ya kuingia ndani na kuyatazama kwa uzuri.

Maporomoko ya Kaporogwe yanapewa nguvu na mto Kala unaotiririsha maji yake kupitia kata ya Isuba na kisha kuendelea na mkondo wake wa asili. Hapo zamani mahala hapa palijulikana kama Kunduriro lakini baadae yalipata umaarufu baada ya mfugaji aitwaye Kaporogwe kutumbukia katika maporomoko hayo.

Kaporogwe inafaa sana kwa picnic, kuogelea, picha, na matembezi. Pango la Kaporogwe linaweza kuingiza hadi watu 150. kivutio hiki pia kipo chini ya halmashauri ambao wanawajibika kukihudumia na kutoa tozo kwa wageni.


Muonekano wa maporomoko ya Kaporogwe kutokea nje

4. Lake Kisiba

Kilomita 18 tu kutokea mji mashuhuri wa Tukuyu lipo Ziwa la volkano linalojulikana kama Ziwa Kisiba au Ziwa Kisiba Masoko au Ziwa Masoko. Lipo katika kijiji cha Masoko.

Mji wa Masoko uliopo Rungwe unaonekana kuwa mji mkongwe kutokana na masimulizi lakini hasa kwa majengo yaliyopo ambayo yalitumika kama ofisi za serikali zote mbili za kikoloni (Ujerumani na Uingereza) kuanzia miaka ya 1886. Mji huu unapewa nakshi na asili ya tamaduni zake, maumbile ya ardhi, uoto wa asili na muonekano wa milima ukiwemo mlima Rungwe. Katika mji huu ndipo linapopatikana Ziwa Kisiba ambalo wengine huliita Ziwa Kisiba Masoko au Ziwa Masoko.

Ziwa Kisiba ni ziwa la volkano ambalo kisayansi limetokana na mlipuko wa volkano, lina upana wa mita 600 na kina chenye mita 70. Ziwa hili ni salama kwa kuogelea na michezo mingine ya ziwani kama Boat Cruising, Camping, Sport Fishing na mingine mingi.

Haya ni manejo manne yanayoweza kutembelewa kwa siku moja. Kwa maswali au maoni tuandikie kupitia anuani hapo chini

Makala hii imeandikwa na Shah Mjanja.

Shah Mjanja ni mpiga picha wa muda mrefu, muandishi na mtayarishaji wa makala za televisheni na filamu, mhifadhi, mwanamuziki na msafiri. Shah Mjanja ni muanzilishi wa Everyday Mbeya na Studio Native.

Shah Mjanja ni Ofisa wa Habari za klabu ya Mbeya City FC.

Mawasiliano:

Simu: +255-682-326410
Barua Pepe: shah@everydaymbeya.com

Work Address
Posta House, FL
Posta Street/Lupaway road
Box 312
Mbeya Town

ONYO: Picha hizi zina hatimiliki, hauruhusiwa kutumia bila idhini ya mmiliki.