Hello Everyday!

Mkoa wa Ruvuma umeniachia kumbukumbu tele na mojawapo ni hii ya Simba wa Vita Baraka Mfaume Nyirenda tunayemfahamu kama Rashid Mfaume Kawawa. Fahamu kuwa hapa wilayani Songea kuna hadithi nyingi zenye masimulizi tele kuhusu mambo ya kale na matukio yake. Yapo makumbusho muhimu kabisa ya Majimaji yaliyo chini ya usimamizi wa Makumbusho ya Taifa na mengine ya Simba wa Vita Kawawa . Leo tena kwa tahfiki zake Rabana na Satari Mola wetu Msitiri nimepata nafasi ya kutembelea makumbusho spesheli ya Mzee Kawawa ambayo yako nyumbani kwake hapa mtaa wa Kawawa kata ya Bombambili wilayani Songea mkoani Ruvuma.

Kwa ufupi Mzee Rashid Mfaume Kawawa alizaliwa Mei 27 mwaka 1926 huko Songea. Alisoma Tabora Boys na kisha baadae akafika huko Makerere, akafanya kazi katika serikali ya kikoloni na kisha baadae akaja kuwa mwanasiasa mkongwe nchini. Alikua mbobezi sana katika mambo mengi, aliongoza migomo mingi ya wafanyakazi katika serikali ya kikoloni na alitengeneza mifumo imara ya kuendesha vyama vya wafanyakazi.

Hii ni nyumba aliyoishi Mzee Kawawa mwenyewe akiwa na familia yake wakiwemo wake zake wawili Sophia na Asina, watoto wake na ndugu zao. Fahamu kuwa nyumba hii aliijenga mwaka 1974, aliitumia kwa shughuli za Serikali, Chama na familia. Hapa ndani pana kumbukumbu tele zenye maana sana, kwa Taifa na Chama cha TANU.

Hapa nyumbani kwa Mzee Kawawa pana kumbukumbu nzuri za mali, vitu, nishani, na vyote alivyotumia Mzee Kawawa enzi za uhai wake alipokua akiishi hapa. Kuanzia thamani za ndani, vitabu vya dini, na vitu binafsi. Makumbusho ya Taifa wanairekebisha nyumba hii kwa sasa na ikiisha kufunguliwa itakua sehemu muhimu sana kwa kujifunza harakati za ukombozi wa Afrika na maisha ya Mashujaa wetu.

Kwangu mimi binafsi nikilinganisha na sehemu zingine nilizo-tembelea; ukiondoa nyumba ya Binti Zaituni hapo Soko Matola ambapo Mwl. Nyerere alikua akifikia mara kwa mara, hii nyumba ya Mndendeule Mzee Mfaume Kawawa ni nyumba ya kihistoria.

“Rashid Mfaume Kawawa ni kiongozi wa nchi changa, ndogo. Lakini ni kiongozi adhimu sana. Ana moyo wa ajabu… Katika TANU alikua anaitwa Simba wa VITA. Haogopi maamuzi mazito. Mkisha kufanya maamuzi, wengine baadaye wanaweza kusita kuyatekeleza, au wanaweza kuyatekeleza kwa shingo upande; na hasa kama walikua hawayapendi. Siyo Rashid Kawawa. Yeye mkisha kufanya maamuzi ya pamoja, atayatekeleza kwa moyo wake wote na uwezo wake wote. Kwa ajili hiyo mara nyingi amebeba lawama peke yake kwa maamuzi ambayo yamefanywa na uongozi mzima wa chama au serikali kwa pamoja, au ambayo nimefanya mimi’.

– Mwl. Nyerere katika mkutano mkuu maalumu wa CCM TAIFA 1990.

Nini maana ya jina Kawawa?

Baba yake Mzee Kawawa alikua moja ya wawindaji bora kuwamo nchini Tanganyika kwa wakati huo. Fani hii ilimpatia nafasi katika serikali na kujipatia umashuhiri, hii ilimfanya asafiri kikazi kila mahala na ilisaidia sana kumjenga Mzee Rashid Mfaume Kawawa kuifahamu vema Tanzania na tabia za watu wake. Fahamu kuwa, mtembea bure si sawa na mkaa bure.

Neno Kawawa kwa lugha ya kwao lina maanisha Muwindaji.

 

Picha ya juu hapo inamuonesha Mzee Kawawa ambaye ni baba yake Rashid Mfaume Kawawa. Baba yake alikua muwindaji bora sana, hata kuna wakati Simba walisumua sana kijijini kwao na yeye alienda na simba hao wakakimbia. Katika mambo mengi mazuri niliyofurahia hapa ndani mojawapo ni nafasi niliyopata ya kulalia kitanda cha Mzee Kawawa walau kwa sekunde 5, lakini pia nimeikuta mashine ambayo Mzee Kawawa aliitumia kuoneshea sinema zake.

Mzee Kawawa alikuwa Waziri wa Ulinzi na anakumbukwa sana katika jitihada zake za kuanzisha Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Mgambo. Mwalimu Nyerere alimuamini sana Kawawa hasa katika utekelezaji wa mambo muhimu ya Taifa ambayo viongozi wengine waliogopa. Fahamu kuwa hata baada ya mapinduzi ya Zanzibar, Mzee Karume alipokuja Tanganyika kuomba Zanzibar na Tanganyika ziungane, mtu wa kwanza kuonana naye alikua ni Rashid Mfaume Kawawa kwa wakati huo akiwa ni Makamu wa Rais wa Tanganyika. Ni Kawawa ndiye aliyempeleka Mzee Karume kwa Mwalimu Nyerere na kisha mazungumzo kuhusu muungano yakaanza.

Fahamu kuwa Mzee Kawawa ndiye mtanzania wa kwanza kucheza sinema hapa nchini na anazo tuzo kadhaa ikiwemo ile ya heshima aliyopatiwa na Tamasha la filamu la Zanzibari. Kawawa ameigiza filamu tano ikiwemo Muhogo Mchungu iliyotoka Julai 1954 na zingine zilizojulikana kama Meli inakwenda, Chalo Amerudi, Wageni Wema na Juma Matatani.

Sinema hızı zilitengenezwa na serikali ya mkoloni zikiwa na lengo la kuleta mafunzo kwa wananchi kuwa maisha ya kijijini yenye kazi ni muhimu kuliko maisha ya mjini ya kuhangaika. Miradi ya sinema za kikoloni ilisimama mwaka 1954 kutokana na gharama za uendeshaji na ni dhahiri kuwa hata sasa katika filamu bajeti nzuri ndiyo huakisi sinema nzuri.

Ukimuacha Osmane Sembene wa Senegali tunayemtambua kama Baba wa Filamu Afrika, basi Mzee Kawawa Simba wa Vita anabaki kuwa na heshima tukufu katika sinema na ukombozi wa Afrika.

Tanganyika na Mzee Kawawa kwa ujumla zimesaidia sana ukombozi wa nchi za Afrika na hapa nyumbani kwake Bomba-Mbili palikua ni sehemu muhimu ya mikutano ya Siri ya kupigania uhuru; mojawapo ikitumiwa kwa ajili ya mipango na mbinu za kujifunza njia za ukombozi dhidi ya watawala wa kigeni huko Msumbiji.

Wapiganaji wengi wa Msumbiji wamefunzwa mbinu za kivita hapa Songea, na baadhi ya viongozi waandamizi wa Uhuru wa Msumbiji akiwemo Mzee Samora Machel mwenyewe walifika hapa na kuhudhuria vikao.

Mwl. Nyerere amefika hapa pia, kwahiyo, yapo mahandaki mengi ambayo chini yalikua na chemba za mikutano, sehemu za chakula na kadhalika.

Hii picha inaonesha nikiingia ndani ya handaki nyumbani kwa Mzee Kawawa. Kiukweli nilijisikka kama Mzee Kawawa mwenyewe au wapiganaji wengine wa wakati huo wakati nilipokua naingia hapa chini. Hili ni moja ya mahandaki yaliyopo hapa Bomba-Mbili kata ya Kawawa nyumbani kwa Mzee Kawawa. Mahandaki haya yamejengwa kwa ustadi mkubwa na umakini kiasi cha adui asiweze kujua wapi yalipo na njia zake za kutokea. Sehemu mojawapo ya kuingia kafika handaki ni chini ya kitanda cha Mzee Kawawa. Hivi vitu vyote humu ndani ni ‘authentic’, yaani ni vitu halisi vya mzee na si vya mfano.

Kitabu cha Quran tukufu alichokua akitumia Mzee Kawawa

Fremu ya picha ya Mzee akiwa na mkewe katika siku mojawapo za hafla.

Sebule mojawapo ya Mzee Kawawa

Hii ni sebule kuu ya Mzee Kawawa na alipenda kukaa hili kochi la kwanza kushoto ambalo lilitazama moja kwa moja mlango wa kutokea nje. Ukutani unaweza ona picha yake akiwa na mkewe wakitoka dansi Fahamu kuwa Mzee alikua msanii na alipenda sanaa. Hii picha imewekwa na makumbusho hivi karibuni.

Ni dhahiri shahiri Mzee alisakata rhumba na alikua romantic sana enzi zake, mbali na kuwa mwanasiasa na kiongozi wa kutegemewa lakini Mzee Kawawa alikua mtu wa matukio kwa namna nyingi sana. Mzee alikua na wake wawili na baadae uzeeni akiwa na umri takribani miaka 70 hivi alioa mke wa tatu.

Uani kwake hapa Bomba-mbili amegawa mara mbil, huku kwa Bi. Mdogo huku kwa Bi. Mkubwa. Aliwezaje kufanya yote hayo kwa familia na Taifa?

Safi! Heko kwa Mzee Kawawa, naye Mwenyezi amsitiri ampatie mapumziko mema.

Bombi Nyumbi!

Makala hii imeandikwa na Shah Mjanja.

Shah Mjanja ni mpiga picha wa muda mrefu, Muandishi na Mtayarishaji wa makala za televisheni na filamu, Mhifadhi, Mwanamuziki na Msafiri. Ni muanzilishi wa Everyday Mbeya na Studio Native.

Shah Mjanja ni Ofisa wa Habari za klabu ya Mbeya City FC.

Mawasiliano:

Simu: +255-682-326410
Barua Pepe: shah@everydaymbeya.com

 

Tazama wimbo huu wa Marijani kusindikiza usomaji wako wa makala haya