Tripophobia – The fear of not having any travel trip currently booked.

Waswahili wana misemo mingi lakini unaotuhusu leo ni ule wa ‘Mtembea bure si sawa na mkaa bure’, ndio, yule akaaye tu hawezi kuwa sawa na yule anayechukua muda wake na kudhurura.

Hello Travellers, nimerejea tena na makala zangu za uzururaji na bila kuwepo na shaka umepata kuzipitia kadha wa kadha huko nyuma, leo ninakusogezea mpangilio mwepesi wa kusafiri ambao huenda hautohitaji gharama kubwa kama ambavyo unaweza kuona katika mipangilio mingi ya safari.

Dunia ina mandhari nyingi sana zinazovutia na kadiri unavyotembea zaidi ndivyo unavyojiridhisha kuwa maumbile ya ardhi yanavutia mno. Mola wetu Mbobezi aliumba dunia kwa namna ya ajabu na kisha akaipa anga inayovutia, lakini maeneo haya yote mazuri hayapo sehemu moja na hayakusubiri, kila eneo la ardhi duniani linashangaza kwa namna ya aina yake. Hebu tutazame Tanzania, Mlima Kilimanjaro upo Moshi, Ziwa Tanganyika lipo Kigoma, Magofu ya kale yapo Kilwa, Ziwa Ngosi lipo Mbeya na kadhalika. Kisha nenda duniani kwa mfano, Everest ipo Asia, Stonehenge ipo Uingereza, Taj Mahal ipo India, Victoria falls lipo Zambia/Botswana, Piramidi zipo Misri na kadhalika, blah blah blah!

Mgawanyiko huu wa mandhari unaifanya dunia iwe nzuri kila sehemu lakini pia unaifanya dunia iwe aghali kuitembelea. Fikiria usafiri, chakula, malazi na tozo za mahala husika! Hivyo, leo ninakuletea mpangilio rahisi wa kutembelea maeneo mbalimbali kwa gharama nafuu zaidi. Gharama pekee utayohitaji ni marafiki, na yupo asiye na rafiki? Hapana, tunao wengi.

Katika makala haya nitatoa mfano kwa kutumia fukwe za Matema zilizopo ziwa Nyasa hususani kupitia safari yangu na wenzangu tuliyoifanya hivi karibuni, na kabla sijaanza hebu nikupe takwimu za ziwa hilo.

Ziwa hili lina urefu wa kilomita 550 na upana wa kilomita 75 na katika baadhi ya sehemu lina kina chenye urefu wa mita hadi 500. Hili ni ziwa la pili kwa kina kirefu Afrika na la nane dunia yote. Lina utajiri wa samaki wengi kuliko maziwa mengi zikiwemo aina zaidi ya 1000 za Mbassa pekee. Hili ndilo ziwa pekee duniani lenye maji freshi ambalo lipo pembezoni mwa milima (Livingstone). Ziwa hili linapatikana katika chi za Tanzania, Msumbiji (Lake Niassa) na Malawi (Lake Malawi).


Fukwe za Matema, Ziwa Nyasa.


Samaki Mbassa

Sasa, ili uweze kusafiri kwa kawaida yapo mahitaji muhimu ambayo ni lazima uweze kuyakidhi, mfano Usafiri, Chakula na Malazi. Kampuni za Utalii zinaweza kukutoza hadi 850,000/- kwenda Matema, mlo mmoja huenda ukafika hadi 20,000/- huku Malazi yakifikia 120,000/- kwa usiku mmoja. Ukijumlisha hesabu hizi unaweza kukuta ili tu kufika Matema na kulala kwa usiku mmoja utatakiwa usipungukiwe 850,000/-,

Je, fukwe zitafaa kwa siku moja? Basi hii ndio sababu iliyofanya nikuandikie makala haya.


Muonekano wa milima ya Livingstone kutokea fukwe za Matema

Mimi na rafiki zangu tunacho kikundi kidogo katika mtandao wa whatsap, kikundi hiki tunakiita ‘Extreme Adventure’, kundi hili halina akaunti benki, wala ofisi na kitu pekee kinachotuunganisha ni hamu za kusafiri. Kundi letu hili lina marafiki ambao tumekutana na tunaelewana kiasi katika mazungumzo, na kwa kiasi wengi tulikutana katika safari zinazoandaliwa na www.everydaymbeya.com. Kundi letu lina members nane, na tulianza polepole, watatu hadi sasa tuko nane. Wakati wa safari members wanayo ruhusa ya kualika marafiki zao ambao hawapo katika kundi.

Kundi letu husafiri kwa gharama za kuchangishana (shared costs), na huu ndio mango nafuu unayotusaidia wakati wote tunapoamua kusafiri. Vilevile, members wanayo ruhusa ya kualika wake zao au watoto wao pale tutapoona wanafaa kuja katika safari husika.


Matema Beach View

Zipo fukwe nyingi katika ziwa Nyasa hapa Matema, sisi hupenda sana kutembelea fukwe ya Lutheran inayoitwa pia Matema Beach View.

Huwa tunaweka idadi ya siku, mfano safari ya Matema huwa tunaweka siku mbili na mchana tatu [3 days 2 nights] kisha tunapiga mahesabu ya usafiri, ada/tozo za malazi na chakula. Ili kukwepa gharama za rejareja huwa tunachanga gharama zote hizo na kuandaa mahitaji wenyewe yatakayotukidhi kuanzia Ijumaa jioni hadi jumapili jioni tukiwa ufukweni.


Muonekano wa Camping yetu ya mwisho

Usafiri

Kwa pamoja huwa tunatafuta gari tutakayotumia kwa ajili ya safari, mfano ili kusafiri kwenda matema utahitaji gari ili uweze kusafiri kilomita 163 kutokea Mbeya Mjini hadi Kyela zilipo fukwe za Matema. Iwapo gari moja haitoshi huwa tunaongeza gari ingine na gari hizi huwa ni zile za marafiki zetu. Kutumia gari za marafiki kunaondoa gharama ya kukodi usafiri kutoka katika gari za kampuni ambazo hizo huwa ni aghali sana. Kwenda Kyela gari hukodishwa kwa 400,000/- na iwapo gari itakusubiri hadi kesho utahitaji kulipa hadi 600,000/-, sasa fikiria kwa siku 3 itakua kiasi gani?

Safari hii tulitumia gari mbili, mojawapo Landrover Defender tuliyoiwekea lita 30 ili kwenda na kurudi. Gari ingine ilikua Toyota Brevis ambayo iliwekewa pia lita 30

Kwahiyo, kwa siku 3 usafiri tulitumia 174,000/- pekee.

Malazi

Mara nyingi tunapotembelea fukwe za Matema huwa tunalala katika tents zetu za nje. Hii inafanya tuepuke ile gharama ya malazi katika vyumba vya hoteli. Gharama pekee tunayolipa katika malazi huwa ni Camping fee ya shilingi 10,000 pekee kwa kila mtu. kwahiyo, kwa watu 7 tunaweza kukaa fukweni kwa siku zote hizo tatu kwa gharama ya 70,000/- pekee.

Gharama za malazi fukweni huenda zikafika 120,000/- kwa chumba.


Turubai za kulala na za kupumzikia.


Beach Cinema

Huwa tunabeba mziki kwa ajili ya burudani. Landrover hutusaidia umeme kwa ajili ya vifaa vyetu zikiwemo simu au sinema. Lakini pia huwa ni sehemu ya kuhifadhia vitu vyetu vya thamani au vile ambavyo hatuvitumii.

Eneo la fukwe za matema huwa halina mwanga wakati wa usiku hivyo huwa tunachukua taa za sola ili kuweza kupata mwanga maeneo ambayo tumeweka vifaa vyetu ikiwemo tents, gari na vifaa vya jikoni. Hii huwa inaongeza usalama lakini pia ni tahadhari kuwa eneo husika wapo watu wanatumia.

Chakula

Ili tupate ile experience nzuri ya camping huwa tunasafiri na vifaa vyote muhimu vya upishi pamoja na chakula chote tutachohitaji tukiwa fukweni kwa siku zote hizo. Mahitaji tunayonunua mara nyingi huwa ni nyama, unga wa ugali na ngano, mafuta ya kupikia na viungo. Huwa tunachukua pia majiko na vifaa vya kupikia zikiwemo sufuria, sahani na vijiko. Pia huwa tunanunua kuku ambao tayari wameandaliwa.

Huwa tunachukua na Cooler Box kwa ajili ya kuhifadhia vyakula vyetu vikiwemo na vinywaji. Tunapotoka mjini huwa tunanunua mahitaji yote muhimu ambayo hayapatikani fukweni, lakini wakati wowote tukiwa na upungufu rafiki yetu mkaazi hutusaidia kununua mahitaji jirani na fukwe.

Safari hii ya watu 7 kwa siku 3 za fukweni tulitumia 205,000/- kununua mahitaji ya chakula na vinywaji zikiwemo nyama, unga, mafuta, na samaki. Pia, wakati wa safari members hutoka nyumbani kwao na vitu vingine mfano chachandu, mayai kiasi na vingine.


Maandalizi ya supu asubuhi ya jumamosi

Huwa tunatengeneza ratiba ya chakula na wapishi wa zamu, kwa siku tatu na usiku mbili maana yake tutakula breakfast 2, lunch 2 na dinner 2. Hivyo ratiba hutengenezwa ya nini kiliwe lini na nani apike chakula husika.


Mambo hayo ufukweni

Inapofika siku ya mwisho ambayo huwa ni jumapili, asubuhi huwa hatupiki breakfast na badala yake huwa tunaenda kijijini/madukani hapo hapo Matema ili kula chakula mgahawani. Hii hutupa fursa ya kujionea chakula cha wakaazi lakini pia kufahamu mji wao vizuri. Huwa tunatumia nafasi hii kununua zawadi kama mchele, vyungu na mahitaji ambayo tunaweza rejea nayo nyumbani kwetu.

 

Matema ni mji mdogo wenye watu wengi na kwa hapa Mbeya sisi tunapaona kama Bagamoyo yetu, pana masoko ya samaki na baadhi ya mali zinazotengenezwa na wakaazi wa huku mfano mikeka, mahitaji ya nyumbani, na chakula pia. Kufanya matembezi kijijini asubuhi ya jumapili hutuunganisha na wakaazi na tamaduni zao.


Wali-ndondo ni sehemu ya breakfast ukiwa fukweni matema.


Nyama choma

Ijumaa jioni na jumapili mchana huwa tunachoma nyama au samaki, rafiki yetu festo ni mvuvi na hutuletea samaki wazuri wakiwa freshi kutoka ziwani.


Mantula, samaki jamii ya perege.


Katika safari zetu chakula huwa ni sehemu muhimu sana, kuanzia kupika kwa kupokezana, kula kwa pamoja na kufurahia ladha ya wapishi tofauti tofauti ni kitu ambacho siku zote kinatupa raha ya safari.

Kwa 205,000/- pekee tuliweza kula na kunywa kwa siku tatu tukiwa watu saba ufukweni, hii gharama ni nafuu zaidi kwa wasafiri.

Sababu muhimu zinazotufanya tusafiri hadi Matema ni mapumziko yetu binafsi, na safari hihi huwa tunazifanya walau kila baada ya miezi mitatu. Safari hizi hutupa muda wa kupumzika na kujadili issues kadha wa kadha zinazotuhusu kama wakaazi, wazawa na wanafamilia.

Tukiwa ziwani muda mwingi tunautumia kuogelea, kucheza muziku na kulala. Pia huwa tunapata muda binafsi kwa ajili ya issues zinazotukabili kama akina baba au akina mama, kila kundi kwa muda wake.

Well, ni matumaini yangu kuwa makala haya yamekuongezea ufahamu katika mtindo wa kusafiri kwa gharama nafuu. Lakini zaidi nimekuonesha namna gani unaweza kutumia faida ya marafiki kuzurura pamoja kwa kuchangia gharama za safari yakiwemo malazi, usafiri na chakula.

Wasalaam,

Makala hii imeandikwa na Shah Mjanja.

Shah Mjanja ni mpiga picha wa muda mrefu, Muandishi na Mtayarishaji wa makala za televisheni na filamu, Mhifadhi, Mwanamuziki na Msafiri. Ni muanzilishi wa Everyday Mbeya na Studio Native.

Shah Mjanja ni Ofisa wa Habari za klabu ya Mbeya City FC.

Mawasiliano:

Simu: +255-682-326410
Barua Pepe: shah@everydaymbeya.com

 

Kama kawaida yetu, nakuachia wimbo wa Madilu System uitwao Aminata. Wimbo huu ni mojawapo wa rekodi zake za mwisho kabla ya umauti kumfika, huenda hata yeye mwenyewe hakuweza kuitazama video hii. Basi na ukuliwaze baada ya kusoma makala haya.

Hadi wakati mwingine…