• Kihistoria Wanyakyusa waliitwa Wakonde
  • Kuanzia utotoni Wanyakyusa wengi walikua na hofu ya uchawi
  • Wanyakyusa huwatazama wachawi kwa jicho tofauti

Kabla ya mambo mengi kubadilika kutokana na tamaduni kuingiliana, wanaume Wanyakyusa wenye umri kati ya miaka 30 na 50, pamoja na wake zao na watoto wadogo, waliishi kwa pamoja katika vijiji. Ni kama vile walikuwa na dini yao wenyewe. Dini ya watu hawa ilionekana katika mila na desturi walizozifuata, kama vile kufanya matambiko. Kulingana na historia ya kabila hilo iliyosimuliwa kwa njia ya mdomo, asili yao inaweza kufuatiliwa hadi kwenye mzizi wake kwa Malkia wa kale wa Wanubi aliyeitwa Nyanseba, ambaye alitekwa na askari wa vita. (Source: One Thousands Languages: Living, Endangered and Lost)

 

Kwa ujumla Wanyakyusa kijadi wanafikiriwa kuwa wanahusiana na Wakinga ambao walitawanyika kuelekea magharibi kama wahamiaji. Wakinga ni kabila la watu wa Tanzania wanaoishi hasa katika mkoa wa Njombe, wilaya ya Makete inayopakana na Mbeya.
Hata hivyo masimulizi mengine yanasema Wanyakyusa wana uhusiano na Waluguru.

Viongozi wao, kama machifu, walipewa sifa za uweza wa kimungu. Washauri wa Chifu hawakuwahi kuwa jamaa zake, bali ni watu wa kawaida tu, wasio wa urithi  wenye mamlaka makubwa juu ya Chifu. Wanyakyusa ni miongozi mwa watu walipambana sana na maisha na mafanikio yao yalitegema juhudi za mtu binafsi. Biashara ya utumwa haikujulikana sana Unyakyusani mwaka 1892, ingawa biashara hiyo kwa hakika ilikuwepo karibu maeneo ya Konde ya Karonga, kwa upande wa Malawi.

Waliishi katika milki ndogo za kichifu, si katika vikundi vya watu vya ukoo, bali katika vikundi vya wazee wenza, wakijaribu kuishi kwa kupatana kuepuka balaa. Wanyakyusa walikua wakulima wenye uchu, walibadilisha mazao mahindi, mahawagwe, maboga, mtama, viazi vikuu na mazao mengine kadhaa huku mashamba ya mazao ya migomba yakiwa yameenea karibu eneo lote wanaloishi.


Kusafisha na kulima shamba kwa saa tatu hadi nne kwa siku lilikua jukumu la wanaume na watoto wao, si wanawake. Mazao hayo yalitumiwa kama chakula, pombe na kuwakirimu wageni, na pia kuuza na kubaidlishana mali kwa sababu enzi hizo hakukuwa na fedha.

Uzee au Ukuu Fulani katika familia au ukoo haukua udhuru wa kutolima shambani, kila mwanaume aliwajibika. Kila mwaka mwanzoni mwa msimu wa mvua, Wanyakyusa walikuwa wakikusanyika mahali palipoitwa ‘Chikungu’ ambapo chifu wao Kyungu anaitisha mvua. Wanakijiji wote waliambiwa wasiwashe moto katika nyumba zao asubuhi ya siku ya sherehe ya kuitisha mvua. Wanakijiji wote walingojea moto mtakatifu kutoka kwenye kaburi liitwalo ‘moto ufya ugawiwe’.

Usuluhishi katika migogoro na rafiki au jirani ulikuwa unachukuliwa kwa umuhimu wa juu sana. Kiongozi  hakuwa na uwezo wa kutekeleza uamuzi na kulipokua na nia ya kusuluhisha ugomvi, ilichukuliwa kuwa inafaa zaidi kufikia suluhu kupitia maoni ya wengi. Mila mara chache zilitaja vita, ingawa migogoro ya mipaka ilikuwa ya kawaida na ingeweza kusababisha mapigano. Wawindaji, si wapiganaji walikuwa mashujaa na waliwinda kwa ajili ya ulinzi wa maisha na mali, ingawa kwa uchaguzi wa silaha ulionesha pia kwamba walipanga vita.

Ingawa walikuwa wanakwepa sana kutaja vita, Novemba 1893 kulikuwa na ugomvi wa mpaka na kisha mapambano yakaibuka na kusababisha vifo vya wanaume sita wa upande mmoja na mmoja wa upande mwingine. Kuhusu mapambano hayo, mwandishi Bridgette Kasuka katika ukurasa wa 158 wa kitabu chake, ‘Malawian Writers and Their Country’ anamnukuu mmisionari Nauhaus akisema kwamba msuguano huo haukutiwa vita, “Niliambiwa hutokea tu ili kuwe na kitu cha kuzungumza”.

Nje ya uchifu wa Wanyakyusa dunia ingeweza kuwa mahali hatari. Safari ya maili 25 ingeweza kuchukua siku tatu kwa sababu ya hitaji la kusafiri mara kwa mara na kupumzika mara kwa mara. Hali hiyo si tu kwamba kullikuwa na vijiji vyenye watu wasio rafiki, bali pia kwa sababu chui, tembo, nyati, viboko, mamba na wanyama wengine walikuwa wengi.

Inasemekana kuwa kabla ya kuwasili kwa wamisionari Wanyakyusa walitupa au kuwaacha watu wao ‘itago’ wafe.

Imani ya kuwepo wachawi ilikuwa muhimu katika mtazamo wa Wanyakyusa. Iliaminika kuwa watu Fulani waliruka juu ya chatu, wakiwadhuru watu wa mifugo usiku. Wachawi hawa walirithi nguvu zao na chatu kutoka kwa mzazi na uchoyo ndio ulikuwa sababu kuu ta kuwadhuru wanaume na ng’ombe.

Chatu walitamani nyama na maziwa yaliyopatikana kwenye mazishi ya waliouawa.

Baadhi ya watu katika vijiji walikua na uwezo wa kuona na kupigana na wachawi katika ndoto zao na waliitwa ‘watetezi’, muhimu zaidi ni wakuu wa vijiji. Maongo na nguvu za watetezi zilitoka kwenye chanzo kimoja na wachawi. Watetezi walifanya kazi ndani ya sharia na maadili, wakati wachawi walifanya ubinafsi dhidi ya sharia na maadili.

Watetezi walfanya kazi kupitia ndoto za usiku. Walikuwa na nguvu, wakitumia uwezo wao kuwaadhibu wakosaji na kazi yao kubwa ilikua ni kulinda ng’ombe, kwa kuwa wote waliishi kwa kula ndizi, maharagwe na maziwa.

Kuanzia utotoni, Wanyakyusa wengi walikuwa na hofu kubwa ya uchawi ambayo kwa wengine imedumu kwa maisha yote. Mwanamume alipopatikana na hatia ya uchawi angeweza kulazimishwa kuhama kijiji. Mwanamke akipatikana na hatia ya uchawi kwa ujumla alipewa talaka, lakini angeweza tena kuoewa baadaye.

Ni mara chache mtu anayedhaniwa mchawi aliuawa, kwa kuwa mchawi alifaa sana vitani, asingeweza kupotezwa na uchifu. Iwapo kungekuwa na mashaka kuhusu tuhuma za uchawi, ‘umwafi’ ilichukuliwa. Ikiwa, katika kunywa umwafi, mtu hakutapika, alifikiriwa kuwa na hatia.

Walio na shaka walidai kwamba kila familia ilichagua washiriki ambao walitapika kwa urahisi. Wakati fulani vikundi vizima vya watu vilijaribiwa kwa ‘umwafi’ ili kuona shida ilikua inatokea wapi.

Hata hivyo, mwisho wa ambo hayo, kulingana na waandishi mbalimbali wa utamaduni wa kinyakyusa, akiwamo Monica Wilson ambaye mwaka 1959 alichapisha kitabu chake ‘Communal Rituals of the Nyakyusa’, matukio ya mambo hayo mwisho wake ulikuwa ni mwaka 1932.

Baada ya hapo mabaidliko yamekuwa makubwa kutokana na kuchanganyika kwa mila.

Chanzo: Makala haya yamechapwa katika Gazeti la Mwananchi, jumatano ya tarehe 05 mwaka 2021. Picha zilizotumika zimetoka katika vyanzo tofauti mtandaoni.